NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimeiomba Serikali inayoingia madarakani kwa miaka mingine mitano kuhakikisha Sheria ya Usalama barabarani nchini inafanyiwa marekebisho haraka ili kupunguza ajali za barabarani.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka Wahanga wa ajali za barabarani ambayo uadhimishwa kila jumapili ya tatu ya mwezi Oktoba kila mwaka.
Reuben alisema katika kuadhimisha siku hiyo muhimu chama hicho na Mtandao wa Usalama Barabarani unaisihi serikali na watunga sheria kukubali na kupokea mawasilisho na mapendekezo ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria za barabarani zina zoweza kupunguza kabisa ajali.
"Tunawashauri pia wadau mbalimbali waendeleze kampeni za mara kwa mara zinazo wakumbusha wananchi, wakiwamo watembea kwa miguu na madereva juu ya kujilinda na ajali za barabarani," alisema Reuben na kuongeza
"Tunasisitiza pia matumizi sahihi ya kofia ngumu, mikanda na viti au vizuizi vya watoto katika magari ili kulinda usalama wetu na pia tukishauri zaidi madereva kuepuka mwendokasi," alisema
Hata hivyo alisema kwa hapa nchini, ripoti zinaonyesha ajali za barabarani zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari, vikosi vya usalama barabarani na asasi za kiserikali na sizizo za kiserikali katika kutoa elimu husika.
"Kamanda na ofisa Mrakibu Msaidizi wa Polisi Deus Sokoni kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani alinukuliwa hivi karibuni akisema idadi ya ajali, vifo na majeruhi ikiwa ni pamoja na makosa ya usalama barabarani imepungua katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2020.
"Aidha, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Fortunatus Muslimu katika mkutano wake na wanahabari mwanzoni mwa mwaka huu 2020 yeye pia alisema kuwa mwaka 2017 ajali za gari zilikuwa 5578, mwaka 2018 ajali 3732 na mwaka 2019 ajali 2704," alisema
Hivyo basi, Reuben alisema Kwa mwaka 2019 ajali zimepungua kutoka asilimia 35 hadi asilimia 28 huku vifo navyo vikipungua kutoka asilimia 31 hadi asilimia 19.
Aidha alisema siku hiyo ya wahanga ambayo huadhimishwa kimataifa, kila ifikapo Jumapili ya wiki ya tatu ya kila mwaka ya mwezi Oktoba ni kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa ajali za barabarani na kuwaenzi mamilioni ya watu waliopoteza maisha kutokana na ajali.
Naye mhanga wa ajali za barabarani, Abdulaziz Shambe alisema alipata ajali na kukaa kitandani miaka mitatu hali iliyosababisha kukimbiwa na ndugu na mke wake wa ndoa.
"Ndugu zangu walinitenga na mke wangu alinikimbia baada ya kuchoka kunihudumia, ndio maana ninapozungumza suala la ajali nasikia uchungu sana kwani nimekuwa mlemavu ila nimeupata kwa sababu ya hizi ajali," alisema
No comments:
Post a Comment