HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 27, 2020

TANZANIA YAISHUKURU AfDB KWA KUENDELEA KUCHANGIA MIRADI YA MAENDELEO


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afika (AfDB), Dkt. Allex Mubiru wakifurahia jambo wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa J.K.Nyerere Jijini Dar es Salaam. 

 

 

 

 

 Na Farida Ramadhani na Ramadhani Kissimba – WFP Dar es Salaam

 

Serikali ya Tanzania imeishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuendeleza ushirikiano wao wa muda mrefu katika kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ukiwemo mkopo wa masharti nafuu wa dola miloni 140 ulioridhiwa Jumatano wiki hii kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa umeme kutoka mto Malagalasi.

 

Shukrani hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango wakati akimuaga aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini, Dkt. Alex Mubiru ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi katika ofisi ya Rais wa benki hiyo.

 

Dkt. Mpango alisema kuwa mradi huo wa bwawa kubwa la umeme unatarajiwa kuzalisha takribani megawati 49.5 za umeme kwa ajili ya Mkoa wa Kigoma na mikoa ya jirani.

 

Alisema Dkt. Mubiru kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika amesaidia kusukuma fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati hapa nchini na katika miaka miwili aliyokaa hapa, Tanzania imeweza kunufaika na fedha za kutekeleza miradi yenye thamani ya takriban dola bilioni 2.5.

 

 “Miradi mingine iliyotekelezwa na benki hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu jijini Dodoma ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, barabara za mzunguko katika jiji la Dodoma na kituo kikubwa cha umeme cha Zuzu” alisema.

 

Dkt. Mpango aliitaja miradi ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 260 kutoka Manyovu, Buhingwe, Kasulu hadi Kabingu mkoani Kigoma pamoja na mradi wa kuunganisha Mkoa huo na umeme wa gridi kuu ya Taifa kuwa ni miongoni mwa miradi mingine iliyotekelezwa kwa mikopo ya AfDB.

 

Aidha, Dkt. Mpango alimuomba Dkt. Mubiru kufikisha salamu za Serikali ya Tanzania na watanzania kwa ujumla kwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na kubainisha kuwa anaamini Mwakilishi Mkazi atakayeteuliwa atakuja kuendeleza pale walipoishia.

 

Naye aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa benki hiyo nchini, Dkt. Alex Mubiru ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi katika ofisi ya Rais wa benki hiyo, alisema anaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote cha miaka miwili alipokuwa nchini.

 

Aliipongeza Serikali kwa kupiga hatua mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kubainisha kuwa Tanzania inauthubutu wa kipekee linapokuja suala la maendeleo.

 

Alisema kwa niaba ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anaahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania kwa kuendelea kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo.

 

No comments:

Post a Comment

Pages