Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Udhalilishaji wa kijinsia visiwani Zanzibar bado ni tatizo kubwa licha ya kuwepo na jitihada mbalimbali za kupambana na matukio hayo.
Hayo yamesemwa na Afisa kutoka kituo cha mkono kutoka hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, Fatma Ally Haji, alipokua akiwasilisha taarifa fupi juu ya matendo hayo katika mkutano wa siku moja wa wadau wa matukio ya udhalilishaji uliofanyika ofisi za Tamwa zilizopo Wilaya ya kati Tunguu.
Alisema taarifa za matukio hayo si za kuridhisha na kueleza kuwa ipo haja jitihada zaidi kuchukuliwa ili kuweza kukomesha au hata kupunguza matukio hayo.
Alisema haiwezi kumaliza siku bila ya kupokea taarifa ya kubakwa kwa mtoto iwe wa kike ama wakiume na kwamba taarifa hizo zimeanza kuleta hofu kubwa kwao.
Akitolea mfano afisa huyo alisema katika mwezi wa tisa mwaka huu jumla ya watoto 13 wa kiume kutoka maeneo tofauti Unguja walingiliwa kinyume na maumbile na kwa kipindi cha mwezi wa kumi watoto 15 walifanyiwa pia matendo hayo.
Alisema kuna tatizo kubwa ambalo anaamini jitahada za haraka zaidi zinahitajika kuondoa chanagmoto hivyo vyenginevyo matendo hayo yanaweza kuongezeka siku hadi siku.
Hakimu wa Mahakama ya mkoa Vuga mjini Unguja Makame Mshimba alisema kuna matukio hufanyika lakini wahusika huamua kubebana.
Alisema kwa mara kadhaa ameshuhudia akiwa Mahakamani mwanamke anaefanyiwa tendo hilo huieleza Mahakama kuwa yeye hakubakwa bali amefanya kwa ridhaa yake kwa kuwa mwanaume ni mtu wake.
Licha ya uwepo wa mazingira hayo hakimu huyo alisema mtoto yoyote aliechini ya miaka 18 hawezi kuridhia kitu kwa mujibu wa sheria na kwamba bado ushahidi unapaswa kusikilizwa na kuendelea.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa ushahidi katika kesi hizo Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashataka (DPP) Khamis Juma alisema bado kuna changamoto katika suala zima la sheria ya ushahidi.
Alitolea mfano kuwa mhanga wa matukio ya udhalilishaji anapokua mtoto amra nyingi hatakiwi kuonana na aliedaiwa kumfanyia kitendo hicho Mahakamani lakini huonana na wakati mwengine hata kukaa chumba kimoja wakifuatilia kesi.
‘’Kwa mazingira ya aina hii mara nyingi watoto huogopa na kujawa na hofu wanapoona walio waliowafanyika matendo maovu badala yake watoto hao hushindwa kutoa ushahidi’’aliongezea.
No comments:
Post a Comment