HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 16, 2020

Madereva 29 wafungiwa leseni kutokana na kufanya makosa barabarani

Kamanda Msaidizi wa Jeshi la Polisi ACP Mkadam Khamis akiangalia michoro mbalimbali inayohusiana na mambo ya usalama barabarani liyochorwa na wachora katuni kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

 

NA MWANDISHI WETU

JESHI la Polisi nchini limesema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu, jumla ya madereva 29 wamefungiwa leseni zao kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ikiwamo ya kuendesha gari kwa mwendo kasi usiokubalika kisheria.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Kamishna Msaidizi wa Jeshi hilo ACP Mkadam Khamis wakati akizungumza na madereva pamoja na wananchi katika Siku ya kamataifa ya kuwakumbuka watu waliopoteza maisha yao  kutokana na ajali za barabarani iliyoandaliwa na Tanzania Media Foundation (TMF).

Kamanda Mkadam alisema wamechukua uamuzi wa kuwafungia madereva hao leseni hizo ili iwe fundisho wa wengine wanaogoma kutii na kufuata Sheria za usalama barabarani na hatimaye kusababisha vifo vya watu.

"Pia katika kukazia usimamizi wa Sheria tumekuwa tukifanya operesheni mbalimbali za usalama barabarani, kuthibiti makosa hatarishi kama vile mwendo kasi, kupima ulevi, kusimamia madereva kufuata michoro ya barabarani," alisema

Aidha alisema wamekuwa wakitoa elimu kwa wanafunzi mbalimbali nchini na katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu jumla ya shule 5,320 na wanafunzi 592,396 wamepatiwa elimu hiyo.

"Pia katika utoaji wa elimu hii ya usalama barabarani kwa mwaka huu kuanzia Januari hadi Oktoba tumevifikia vijiwe vya bodaboda 11,760, stendi za mabasi  3,589, madereva  wa bodaboda  212,464, idadi ya mabasi 1,182,366 na abiria 6,874,225, wote hawa wamepatiwa elimu na tunaamini kuwa itakwenda kuwasaidia katika kupunguza ajali nchini," alisema

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), Fausta Musokwa alisema mamlaka husika zinapaswa kuwakumbuka waliopoteza maisha kwa kutilia mkazo kwenye maeneo yenye mapungufu, mfano kwenye sheria, tabia na uelewa.

"Pia tuwasaidie walionusurika katika ajali kwa kupaza sauti zao. Tuchukue hatua kwa kushirikiana kwani umoja ni nguvu," alisema  

Aidha alisema ni vema kwa waandishi na vyombo vya habari kuzingatia sheria na misingi ya uandishi kwa kushirikiana na polisi ili kupata taarifa sahihi, kutoa haki ya kujibu pamoja na kuunga mkono juhudi zao kutoa elimu juu ya matumizi ya barabara.

"Pia ni vema waandishi wakatambua kazi na mafanikio yalipo katika mapambano ya ajali za barabarani yanaweza kutumika kufundisha nchi nyingine," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages