HABARI MSETO (HEADER)


 Breaking

December 07, 2020

FORVAC kununua Misaji (Teak) ya shilingi milioni 150


Mratibu wa Kitaifa wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Emmanuel Msoffe akiwaeleza waandishi wa habari waliotembelea Bustani ya Kipiki wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma namna ya kuanda na kupanda mche wa msaji. 

NA SULEIMAN MSUYA, NAMTUMBO


KATIKA kuhakikisha uhifadhi wa misitu na utunzaji wa mazingira unakuwa endelevu Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) inatarajia kugawa miti  miche ya misaji 300,000  itakayogharimu shilingi milioni 150.

Misaji hiyo itagawanywa kwa wananchi na vikundi vya upandaji miti katika Kijiji cha Liuli Wilaya Nyasa mkoani Ruvuma.

Programu ya FORVAC inatekelezwa kupitia Idara ya Misitu na Nyuki chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland.

Kupitia programu hiyo yenye lengo la kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu inatekelezwa kwenye wilaya 12 ambazo ni  Handeni, Kilindi, Mpwapwa, Kiteto, Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Mbinga na Songea zilizopo katika Kongani tatu za Tanga, Lindi na Ruvuma.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali walikuwa kwenye ziara ya kujifunza dhana nzima ya program hiyo,  Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda amesema wameamua kuanzia katika upandaji miche ili dhana nzima ya mnyororo wa thamani ieleweke.

Amesema katika mwaka huu 2020/2021 watagawa miche ya Misaji 300,000 yenye thamani ya shilingi milioni 150 kwa wanavijiji wenye mashamba ya miti wilayani Nyasa.

Mutunda amesema ugawaji wa miche hiyo inayozalishwa kwenye Bustani ya Kipiki iliyopo Shamba Miti Mpepo ni mwendelezo wao wa kuhakikisha wananchi wanashiriki kutunza mazingira.

"Utaratibu huu wa ununuzi wa miche umeanza mwaka jana ambapo tulinunua miche 150,000 yenye thamani ya shilingi milioni 75.

Mwaka huu tutanunua miche 300,000 inayogharimu shilingi milioni 150 kwani tunaamini mnyororo wa thamani unaanzia kwenye mbegu, miche na baadae miti," amesema.

Amesema iwapo miti hiyo 300,000 itafanikiwa kuota na baadae kuvunwa itapunguza uharibifu wa misitu ambao unaonekana kuongezeka hasa maeneo ambayo hayana Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).

Mratibu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe, ambaye pia ni mtaalam wa miti amesema miti ya Misaji ni fursa nzuri ya kibiashara inayopaswa kupewa kipaumbele.

Amesema iwapo kila mkulima wa miti atajikita kwenye upandaji wa Misaji ukataji wa miti kama Mninga, Mkongo na mingine utapungua.

"Promosheni tunayofanya ni kuhamasisha upandaji Misaji inatokana na ukweli kuwa inafaa kutumika kwa ajili ya utengenezaji wa thamani, kuweka sakafu, kutengeneza deki za meli na majahazi, kupaulia na wengine kutumia kama kuni," amesema.

Msoffe amesema ili miti hiyo kuvunwa inachukua muda wa miaka 25 hadi 30 kwa Tanzania ila kwa nchi za baridi hadi kufikia miaka 60,"amesema.

Mtaribu huyo amesema miti hiyo inakubali katika ardhi zenye kina kirefu na rutuba na maji mengi kama Longuza Tanga, Mtibwa na Kilombero Morogoro, Namtumbo na Nyasa Ruvuma.

Kwa upande wake Ofisa Misitu Mkoa wa Ruvuma, Africanus Charles amesema wamepokea kwa furaha FORVAC kwa kuwa imekuja kupambana na mabadiliko ya tabia nchini na kukuza uchumi wa wanavijiji.

"FORVAC wamekuja kutupa nguvu zaidi na sisi tutawaunga mkono kwa nguvu zote ili uhifadhi uweze kuendelea kwani una faida kwa mkoa na nchi.

Tuna bustani za Misaji mbili ambazo ni hii ya Kipiki na Ndongosi ila pia  kuna bustani ya miche ya Pine na Mikaratusi," amesema.

Ofisa Misitu huyo amesema mkoa umetenga hekta 80,000 ambapo hadi sasa wamepanda asilimia 53 ya lengo na miti ambayo wanapanda ni ya kibiashara.

Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Shamba la Mpepo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, Misana Manumbu amesema bustani ya Misaji katika shamba hilo imekuwa na mafanikio.

Amesema bustani hiyo yenye heka tano wamepanda miti ya Misaji milioni 1 ambapo wanagawa kwa wanavijiji na kuuza kwa taasisi mbalimbali zenye uhitaji.

"Tumegawa miche zaidi ya 200,000 kwa wananchi 100, kule Mpepo tumegawa miche ya Pine 150,000," amesema.

Mhifadhi huyo amesema zoezi hilo la uzalishaji miche linakabiliwa na changamoto ya moto na barabara hivyo kuomba mamlaka kuchukua hatua.

Manumbu amesema uzalishaji wao unakidhi hitaji ya watu wanaotaka miche hivyo iwapo kuna watu wanahitaji wawasiliane nao.

Amesema miti ya Misaji ina thamani kubwa katika soko hivyo kuwataka wanavijiji na wananchi kupanda miti mingi kwa ajili ya vizazi vyao vya baadae.

Manumbu amesema miche hiyo inaweza kupandwa 1,200 katika hekta moja na kwa hekari miche 450 na kwamba wanatoa elimu ya upandaji kwa wanavijiji.

Amesema FORVAC wamekuwa wakipigania uhifadhi hivyo wanapaswa kuungwa mkono na wadau wengine.


No comments:

Post a Comment

Pages