HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 07, 2020

Serikali yataka uwekezaji zaidi mafunzo ya bima

 

 

Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini, Dk Mussa Juma akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya  siku mbili ya watoa huduma za Bima kwa wafanyakazi wa Benki ya NMB iliyofanyika Zanzibar mwishoni mwa juma. Kulia ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi na kushoto ni Afisa Mkuu na Rasilimali Watu, Emmanuel Akoonay.

 

Na Mwandishi Wetu, Unguja


Changamoto za upatikanaji wa huduma muafaka za bima nchini zitapata ufumbuzi kutokana na uwepo na wataamu wenye mafunzo stahiki kwa ajili ya kuzifanyia kazi na kusaidia maendeleo ya sekta hiyo kwa ujumla.


Hiyo ni kwa mujibu wa Kamishna wa Bima, Dkt Mussa Juma, ambaye amewataka watoa huduma hizo wote kuwekeza zaidi katika mafunzo na elimu ya bima kwa wafanyakazi wao ili waweze kulihudumia soko kikamilifu na kusaidia kubuni bidhaa
zinazoendana na mahitaji ya taifa na mazingira ya nchi yetu.
Akiongea hapa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa mafunzo ya maafisa bima wa
 

Benki ya NMB, Dkt Juma alisema uwekezaji huo utayasaidia makampuni ya bima, benki zinazofanya biashara hiyo, mawakala na wadau wengine kuwa na wafanyakazi wenye
sifa za kitaaluma katika tasnia hiyo.
 

Kada hiyo ya wataalamu ni muhimu si tu katika kurahisisha ukataji wa bima na upatikanaji wake bali pia kwenye kusaidia kuwepo kwa bidhaa sahihi sokoni pamoja na kuongeza uwezo wa kuwahudumia wananch. Pia watashiriki kutatua changamoto
zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo mchango mdogo kwenye uchumi na maendeleo ya nchi, alifafanua kiongozi huyo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).


“Sheria ya Bima inataka kila mtoa bima, awe benki au hata wakala yeyote wa bima, anatakiwa kufanya mafunzo kwa watoa huduma wake. Nawapongeza NMB kwa kuzingatia hilo na sisi kama wasimamizi tutahakikisha mnapata msaada mnaotaka ili
kusogezahuduma za bima kwa Watanzania wengi zaidi,” Dkt Juma alisisitiza katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza Ijumaa.


“Kuingia kwa Benki ya NMB kwenye bancassurance ni ushindi mkubwa kwa sisi tulioko kwenye sekta ya bima nchini, kwani tayari kwa miezi michache tu tumeshaanza kuona mabadiriko ya utoaji huduma pia watu wengi wamepata ahueni kwani Benki ya NMB imesambaa kila kona ya nchi hii, bara na hapa Zanzibar,” aliongeza.


Taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini ilianza kutoa huduma za bima mwezi Februari mwaka huu ikiwa ni benki ya kwanza kuanza rasmi kufanya biashara hiyo ijulikanayo kitaaluma kama bancassurance.


Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa NMB, Emmanuel Akoonay, uwekezaji katika mafunzo ya wafanyakazi wa kitengo cha bima umekuwa wa tija kubwa kwa benki hiyo na upatikanaji wa huduma zake.
 

Alisema lengo la kuzindua kitengo cha NMB Bancassurance lilikuwa ni kusaidia kuleta huduma za bima karibu zaidi na Watanzania kwani watu wengi walikuwa hawafikiwa na
huduma hizo. Hilo limefanikiwa kwani watu wengi sasa wanatumia matawi zaidi ya 225 ya NMB na mawakala zaidi ya 8;000 kukata bima hata walio vijijini na maeneo ya pembezoni kabisa huku wengi zaidi wakitarajiwa kuhudumiwa kidijitali, Akoonay alifafanua na kuongeza:


“Tangu kuzinduliwa kwa bancassurance, zaidi ya wafanyakazi 250 wamekwishapokea mafunzo haya na kupewa vyeti. Mafunzo haya yameongeza sana utoaji huduma na hivyo kuwa na wastani wa watu zaidi ya 30,000 wanaokata bima kila mwezi kupitia
NMB.


“Mipango yetu ikishakamilika ya kuanza kutoa huduma za bima kidijitali ikiwemo kupitia NMB Mkononi, watu wengi zaidi wataweza kupata huduma za bima popote pale walipo na wakati wowote na hivyo kutoa kabisa changamoto ya umbali katika kufuata huduma za bima.”


Mwezeshaji mkuu wa mafunzo hayo yaliyowashirikisha pia viongozi na wataalamu kutoka makampuni ya bima yanayoshirikiana na NMB alikuwa aliyekuwa Kamishna wa
TIRA, Dkt Baghayo Saqware.
 

Pia Akoonay alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wafanyakazi wao ili kuendana na mabadiriko yanayotokea sokoni na hivyo kutengeneza timu yenye uelewa
wa juu katika sekta ya bima.
 

Naye Afisa Mwandamizi wa Bima NMB, Martine Massawe, alisema baada ya mafunzo hayo washiriki wataweza kuyafahamu mahitaji ya soko la bima na kuyashughulikia kwa
weledi mkubwa. Baada ya kujua kinachoendelea sokoni kupitia mafunzo mbalimbali, wafanyakazi wa NMB wataiwezesha benki hiyo kuwa mshindani mzuri sokoni.

No comments:

Post a Comment

Pages