Mtafiti kiongozi wa mradi wa kuzalisha migomba kwa njia ya maabara akionesha atua mbalimbali wanazopitia katika uzalishaji.
NA MWANDISHI WETU
KITUO cha Tengeru kilicho chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) iliyopo Tengeru mkoani Arusha kinatarajia kuzalisha mbegu bora za migomba baada ya kupokea kiasi cha Sh.Milioni 400 za ruzuku kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH).
TARI-Tengeru iliyoanzishwa mwaka 2016, imejielekeza katika kuwasaidia wakulima wa mbogamboga, maua na matunda.
Akizungumzia kuhusu uzalishaji huo mkoani Arusha jana,Ofisa utafiti wa TARI-Tengeru, Grace Kindimba amesema ili kufanikisha hilo wanatumia teknolojia ya tissue culture ambayo huwataka kuweka miche ya migomba katika mwanga wenye viwango tofauti hivyo kufanikisha uzalishaji wa migomba 15,000 kila baada ya miezi minne.
Amesema teknolojia hiyo humwezesha mkulima kuwa na migomba yenye ukubwa sawa, isiyo na magonjwa na itakayozaa kwa wakati mmoja.
“Maabara ya kuzalisha miche ya migomba kwa teknolojia ya tissue culture ilianza uzalishaji mwaka 2009 na mpaka mwaka 2018, ilikuwa inazalisha wastani wa miche 2,000 kwa kila miezi minne ingawa uwezo wake wa mwisho ilikuwa miche 5,000”
“Kuanzia Oktoba 2018, maabara hiyo ilianza kufanyiwa ukarabati ili kuiboresha na kuiongezea uwezo ambapo Mradi huo ulipaswa kukamilika Juni 2020”Amesema Kindimba
Kindimba amefafanua kuwa maabara hiyo pia itazalisha miche ya viazi mviringo na wakati huo, utaratibu wa kuzalisha miche ya vanilla, minanasi na viazi vitamu ukiendelea.
Tayari maabara inao uzoefu wa kufanya kazi hivyo kuwanufaisha walengwa wanaojumuisha wafanyakazi wa taasisi hiyo, wanafunzi wa vyuo vikuu, wakulima pamoja na wajasirimali na itaongeza kasi ya utafiti wa kuzalisha mbegu bora za mbogamboga, matunda na viungo vya chakula (spicies).
Kituo cha TARI-Tengeru kupitia kiliomba ruzuku ya kiasi cha Sh.Milioni 400 kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kujenga maabara itakayoiongezea uwezo wa kuzalisha miche mingi zaidi hivyo kukidhi mahitaji ya wateja ilionao.
Kwa kutumia teknolojia ambayo huuongezea mmea uwezo wa kujitengenezea chakula mpaka saa 16 badala ya nane za kawaida, maabara hii iliyofadhiliwa na COSTECH, imeweza kukuzwa migomba kwa haraka hivyo kuweza kupandikizwa shambani ndani ya muda mfupi.
No comments:
Post a Comment