HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 17, 2020

Vifungashio hafifu chanzo cha upotevu wa mavuno ya zao la nyanya - Utafiti

Imebainika kuwa matumizi ya vifungashio duni kwa wakulima wa nyanya ni chanzo cha upotevu wa mavuno ya zao hilo.

Utafiti uliofanywa na Mwalimu wa fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo (Agro –Mechanics) VETA Kihonda, Mhandisi Joseph Kimako umebainisha kuwa wakulima wengi wa nyanya nchini wanatumia makasha ya mbao ambayo husababisha uharibifu mkubwa wa nyanya wakati wa usafirishaji.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti juu ya upotevu wa mavuno katika zao la nyanya (Assessment of Post-harvest losses in tomato production) katika mkutano wa 12 wa Kimataifa wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), uliofanyika tarehe 3 hadi 5 Desemba, 2020, Mhandisi Kimako alisema utafiti utafiti alioufanya katika  wilaya za  Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro umeonyesha kuwa asilimia 63 ya wakulima hutumia makasha ya mbao kusafirisha nyanya kwenda kwenye masoko huku asilimia 37 pekee ya wakulima hutumia makasha ya plastiki. Kasha za plastiki ni salama zaidi kwa kuwa ni laini na huruhusu hewa kupita kirahisi na hatimaye kuzuia uharibifu kwenye nyanya.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kimako, robo ya nyanya zinaharibika baada ya kuvunwa kutokana na changamoto ya vifungashio inayosababishwa na uwezo mdogo wa kiuchumi kwa wakulima kuweza kununua makasha ya plastiki na changamoto ya upatikanaji wa kreti hizo katika maeneo yao.

Sababu zingine zinazosababisha upotevu wa zao hilo kwa mujibu wa utafiti huo ni pamoja na ukosefu wa soko la uhakika la zao hilo mara baada ya mavuno na ukosefu wa elimu ya namna bora ya kupunguza upotevu wa nyanya baada ya kuvuna.

Utafiti huo umeainisha mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hiyo ambayo ni pamoja na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika nyanya katika maeneo yanayolimwa zao hilo, mafunzo kwa wakulima juu ya namna ya kupunguza upotevu wa nyanya wakati wa kilimo na baada ya mavuno pamoja na ujuzi wa kukabiliana na upotevu wa mazao.

Mhandisi Kimako alisema VETA itaendelea kuwasaidia wakulima kwa kuwashauri namna bora ya kupunguza hasara zinazotokana na upotevu wa zao la nyanya kabla na baada ya mavuno pamoja na kubuni vifaa na teknolojia mbalimbali za kusaidia kupunguza changamoto hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages