HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 30, 2020

Wadau walilia mabadiliko ya sheria, kuzika mzimu ajali za barabarani

Wananchi wakishuhudia ajali iliyotokea mwaka 2014. (Picha ya maktaba).


Na Janeth Jovin


DESEMBA 14, 2020 watu 14 walipoteza maisha na wengine 13 kujeruhiwa katika ajali ya barabrani iliyotokea maeneo ya Kiini cha Mkiwa mkoani Singida ikihusisha gari ndogo aina ya Hiace na Lori la mafuta.

Kati ya vifo hivyo, saba vilikuwa ni vya ndugu wa familia moja ambao walikuwa wakitokea Mwanza kwenda mkoani Singida katika sherehe ya harusi.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Sweetbert Njewika akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo alisema kuwa chanzo chake ni uzembe wa dereva wa gari ya abiria ambaye alikuwa mwendo kasi.

Mbali na ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu wengi kwa wakati mmoja, Desemba 21, 2020 Jeshi la Polisi nchini lilitoa taarifa yake ya hali ya usalama kwa kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu.

Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamishna wa Oparesheni na mafunzo CP Liberatus Sabas ameonesha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu, jumla ya watu 1,158 wamepoteza maisha kutokana na matukio ya ajali za barabarani.

Aidha watu 2,089 walijeruhiwa katika matukio 1,800 ya ajali za barabarani yaliyorekodiwa kuanzia Januari hadi Novemba 2020.

Kuendelea kutokea kwa ajali hizo zinazosababisha vifo ni kielelezo tosha kuwa bado kama nchi tunapaswa kuendelea kupaza sauti ili kuhakikisha tunapunguza kabisa au kumaliza tatizo hilo.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2018, ilionesha kuwa asilimia 30 za ajali barabarani katika nchi zilizoendelea hutokana na mwendokasi huku nusu ya ajali katika nchi za dunia ya tatu, Tanzania ikiwemo husababishwa na mwendo kasi pia.

Aidha ripoti hiyo ilionesha kuwa watu 3,400 hupoteza maisha kila siku kutokana na ajali za barabarani na athari zake kwa familia na jamii kwa ujumla ni kubwa, kwani vifo hivyo vya ghafla huacha kovu la milele kwa jamii.

Utafiti huo wa WHO ulionyesha kuwa asilimia 40 hadi 50 ya madereva uendesha magari kwa mwendo kasi zaidi ya kipimo kinachotakiwa, hali ambayo husababisha ajali moja kati ya tatu zinazotokea barabarani kila siku.

Kwa kutambua umuhimu wa kupunguza ajali hizo, mwezi Aprili, 2018 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliamua kupitisha hatua kadhaa ili kuchapusha mchakato wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) yanayohusiana na usalama barabarani.

Miongoni mwa hatua hizo ni kukubali makubaliano ya malengo 12 ya kimataifa ya usalama barabarani na kuanzisha wakfu wa Umoja wa Mataifa wa usalama barabarani.

Hata hivyo kitisho kikubwa cha janga hilo la ajali za barabarani  ni kutokana na asilimia kubwa ya wanaopoteza maisha ni vijana ambao pia ndio nguvu kazi kwa mataifa mengi.

Mercy Kessy ni Ofisa Programu Masuala ya Usalama Barabarani kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), anasema wakati umefika sasa wa kufanyika kwa marekebisho ya sheria ya usalama barabrani ya mwaka 1973 ili kunusuru maisha ya watanzania.

Anasema kwa mujibu wa takwimu hizo za polisi bado watanzania wengi wanapoteza maisha yao kutokana na ajali za barabarani.

Kessy anafafanua kuwa sheria ya sasa dereva anayeendesha gari kwa mwendo kasi kisha akapata ajali na kusababisha kifo kwa vyovyote vile akipelekwa mahakamani uchagua kulipa faini kuliko kwenda jela miaka mitatu.

“Hivyo basi, ili madereva waweze kujutia makosa waliyofanya ni wazi kuwa faini inatakiwa iendane na kosa, ikiwezekana pia sheria iangalie upya viwango vya adhabu vilivyopo ili kuendana na wakati,” anasema Kessy na kuongeza

“Kwa upande wangu sioni kama adhabu zilizopo kwenye sheria zinafanya madereva kutofanya makosa kwa sababu ninavyoona mimi faini ni ndogo na inalipika kwa urahisi, hivyo haiwezi kuzuia dereva asifanye makosa,” anasema.

Kuhusu mwendokasi Kessy anasema “Kifungu cha 51(8) cha sheria ya Usalama Barabarani kinasema mwendo kasi ni Kilomita 50 kwa saa kwenye maeneo ya makazi lakini bado haijafafanua hasa ni maeneo gani ya makazi hiyo speed inatakiwa kutumika,” anasema

Anasema ni vema pakawa na ufafanuzi katika hilo ili kujua mipaka ya hayo makazi kwa maana makazi ya watu yamekuwa yakifuata barabara na ndio mgogoro unapotokea lakini marekebisho yakifanyika na kuonyesha makazi yanaanzia wapi itaweza kupunguza ajali za barabarani.

Vievile Kessy anasema Malengo ya Usalama Barabarani (SDG’s) ya mwaka 2030 yanaweza kufikiwa hapa nchini kama sheria zitaendana na mazingira yaliyopo sasa.

“Sheria tuliyonayo ilitungwa mwaka 1973, leo hii tunaongelea mwaka 2020 ni dhahiri kuwa yapo mabadiliko mengi yamefanyika katika swala zima la miundombinu lakini pia ongezeko la vyombo vya moto, watembea kwa miguu, hivyo ili kufikia malengo ya SDG’s 2030 ni vema tukafanya hayo maboresho ya sheria ili kuendana na mazingira halisi tuliyonayo,” anasema Kessy.

Kessy anasisitiza kuwa sheria iliyopo sasa ni ya muda mrefu hivyo maboresho yanahitajika na kuongeza kuwa wadau mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao nini kifanyike baada ya kuona kumekuwa na ongezeko kubwa la ajali.



Naye Mwanasheria wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Isabella Nchimbi anasema utafiti waliofanya umebaini kuwa sheria ya sasa ina mapungufu kadhaa ndio maana wadau walikutana na kufanya marekebisho.

Aidha Nchimbi anasema mapungufu ya sheria yapo katika sehemu mbalimbali ikiwamo mwendo kasi ambao umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazogharimu uhai wa watu wengi nchini.

“Adhabu zisizokidhi wala kuleta hofu kwa madereva wasiotaka kutii sheria zimeendelea kufifisha juhudi za kudhibiti tatizo hilo la mwendo kasi na hayo ndio mapungufu yaliyopo katika sheria,” anasema.

Anasema kwa ajili ya kuzuia mwendo kasi, sheria mpya itapaswa kuzingatia aina zote za magari na sio magari ya biashara yenye uzito mkubwa na yale yatumikayo kwa usafiri wa umma pekee.

“Kwa ajili ya utekelezaji, sheria iweke mawanda mapana ya kupunguza mwendokasi katika sheria kuu na sio kupitia kanuni zinazotungwa chini ya mamlaka ya Waziri,” anasema

Anasema sheria mpya inayopendekezwa itakapopita itasaidia sana kudhibiti madereva na ajali zitokanazo na mwendokasi maana watekelezaji wa sheria hiyo watapata meno zaidi ya kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), Fausta Musokwa yeye amezitaka mamlaka husika kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na ajali za barabarani kwa kutilia mkazo kwenye maeneo yenye mapungufu, mfano kwenye sheria, tabia na uelewa wa jamii.

"Pia tuwasaidie walionusurika katika ajali kwa kupaza sauti zao. Tuchukue hatua kwa kushirikiana kwani umoja ni nguvu," anasema  

Aidha anasema ni vema kwa waandishi na vyombo vya habari kuzingatia sheria na misingi ya uandishi kwa kushirikiana na polisi ili kupata taarifa sahihi, kutoa haki ya kujibu pamoja na kuunga mkono juhudi zao za utoaji wa elimu juu ya matumizi ya barabara.

"Pia ni vema waandishi wakatambua kazi na mafanikio yalipo katika mapambano ya ajali za barabarani yanaweza kutumika kufundisha nchi nyingine," anasema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Reuben, ameiomba Serikali katika miaka mitano itakayokuwa madarakani  kuhakikisha Sheria ya Usalama barabarani nchini inafanyiwa marekebisho haraka ili kupunguza ajali za barabarani.

Reuben amesema Tamwa inaendelea unaisihi serikali na watunga sheria kukubali na kupokea mawasilisho na mapendekezo ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria za barabarani zina zoweza kupunguza kabisa ajali.

"Tunawashauri pia wadau mbalimbali waendeleze kampeni za mara kwa mara  zinazo wakumbusha wananchi, wakiwamo watembea kwa miguu na madereva juu ya kujilinda na ajali za barabarani," alisema Reuben na kuongeza

"Tunasisitiza pia matumizi sahihi ya kofia ngumu, mikanda  na viti au vizuizi vya watoto katika magari ili kulinda usalama wetu na pia tukishauri zaidi madereva kuepuka mwendokasi," amesema

Hata hivyo amesema kwa hapa nchini, ripoti zinaonyesha ajali za barabarani zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari, vikosi vya usalama barabarani na asasi za kiserikali na sizizo za kiserikali katika kutoa elimu husika.

No comments:

Post a Comment

Pages