HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 11, 2021

BARABARA YA NYAHUA - CHAYA KUKAMILIKA MACHI


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo kwa watalaamu wa Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya AECO  na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora, mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Nyahua – Chaya (km 85.4).


Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora Mhandisi Damian Ndabalinze, akifafanua jambo kwa Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya AECO, Mhandisi Adel Alkhateeb, wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Nyahua – Chaya (km 85.4) kwa kiwango cha lami. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akifatilia.

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa barabara ya Nyahua - Chaya (km 85.4) inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi China Henan International (CHICO).

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Tabora – Nyahua – Chaya – Itigi – Manyoni yenye jumla ya urefu wa kilometa 259 kutapunguza urefu wa safari kwa kilometa 191 kwa magari yanayopitia barabara ya Tabora - Nzega - Singida hadi Manyoni na hivyo kuleta tija kwa wasafiri na wasafirishaji wa mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.

“Hakikisheni sehemu ya kilometa sita zilizobaki kuwekwa lami zinakamilika kabla ya mwezi machi ili kuwezesha wananchi kunufaika na barabara hii”, amesema Mhandisi Kasekenya.

Amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora kuilinda miundombinu ya barabara, madaraja na taa za barabarani ili zidumu kama ilivyokusudiwa.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora Mhandisi Damian Ndabalinze, amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa mkoa huo umejipanga kuhakikisha unalinda barabara zake na kuziwekea taa sehemu nyingi ili kuongeza usalama na kupendezesha mji huo.

Zaidi ya shilingi bilioni 117 zimetumika katika ujenzi wa barabara ya Nyahua - Chaya ambayo imehusisha ujenzi wa madaraja makubwa mawili ya Nyahua na Kizengi ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka huu.

Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Tabora kwa ziara ya siku mbili ya kukagua miundombinu inayoendelea kutekelezwa mkoani humo.

No comments:

Post a Comment

Pages