HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 15, 2021

DKT. NDUGULILE AIPONGEZA TTCL KWA KUJIENDESHA KWA FAIDA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo kwa Mameneja wa Mikoa wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (hawapo pichani) wakati akifungua kikao cha utendaji kazi wa Shirika hilo, Dodoma.  Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Waziri Kindamba.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza kumkaribisha Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyeketi katikati) kabla ya kufungua kikao cha utendaji kazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Dodoma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Waziri Kindamba.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba akifafanua jambo kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyeketi katikati) kwenye kikao cha utendaji kazi wa Shirika hilo kilichowakutanisha Mameneja wa Mikoa wote wa Shirika hilo (hawapo pichani), Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi.

 

 

  

Na Prisca Ulomi, WMTH

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kujiendesha kwa faida na kupunguza hasara kwa kipindi cha miaka mitano na kuacha kuacha TTCL kwa hasara

 

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha utendaji kazi wa Mameneja wa mikoa yote wa Tanzania Bara na Zanzibar wa TTCL na Menejimenti ya Shirika hilo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jeshi la Zimamoto, Dodoma

 

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amemweleza Dkt. Ndugulile kuwa Shirika lake limeweza kujiendesha kwa faida kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2016/2017 kwa kutengeneza faida ya shilingi bilioni tano kwa mwaka tofauti na miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2016 kurudi nyuma ambapo Shirika limekuwa likijiendesha kwa hasara

 

Dkt. Ndugulile ameitaka TTCL kuacha kufanya biashara kwa mazoea bali wawe wabunifu, wafanye utafiti wa masoko ili kubaini mahitaji ya wateja, kuongeza wateja na kwenda sambamba na ushindani kwa kuwa mpaka sasa TTCL ina asilimia mbili ya wateja wa simu za mkononi kwenye soko ukilinganisha na kampuni nyingine na jumla ya wateja milioni 1.3 wa simu za mkononi

 

Amewaita Mameneja wa Mikoa yote ya TTCL nchi nzima ili wajadaliane na kuweka malengo yanayopimika kwa kuwa hivi sasa kiasi cha shilingi trilioni 12 zinazunguka kwenye huduma ya fedha mtandao kwa mwezi na miamala isiyozidi milioni 300 kwa mwezi zinapita mtandaoni ili TTCL itumie fursa hii kufanya biashara na kutoa gawio

 

Amesisitiza kuwa kila Meneja wa Mkoa wa TTCL apewe malengo ya kuongeza wateja, kushughulikia malalamiko ya wateja kwa wakati, kutoa huduma nzuri kwa wateja na kuhakikisha kuwa ukuaji wa kuridhisha wa TTCL unaonekana

 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amewaeleza Mameneja hao kuwa watumie mbinu za kuongeza wateja na kutengeneza mazingira ya kukubalika katika maeneo wanayotoa huduma kama ilivyo kwa waganga wa tiba za asili na wahubiri wa dini ambapo wamejenga imani na wanatoa huduma kwa wafuasi wao

 

Pamoja na kikao hicho, washiriki wamepatiwa mada kuhusu Mkakati wa Kurahisisha Uongozi na Ushirikiano na Ofisi za Serikali Mikoani na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka kwa Johnson Nyingi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na mada kuhusu utawala bora kutoka kwa Apolinari Tamayamali, Mkurugenzi wa Utawala Bora, Ofisi ya Rais – Ikulu

No comments:

Post a Comment

Pages