HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2021

DKT. NDUGULILE AKUTANA NA BODI, TAASISI ZAKE KUJIPANGA KUENDESHA WIZARA MPYA

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi za Wizara yake (hawapo pichani) wakati wa kikao chake na viongozi hao cha kujipanga kuendesha Wizara hiyo kilichofanyika Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na kulia Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Justina Mashiba akisisitiza jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zake, Dodoma. Kutoka kushoto ni Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba.

 

Na Prisca Ulomi, WMTH

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amekutana na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara yake ikiwemo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Tume ya Taifa ya TEHAMA (ICTC) na Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) na Menejimenti ya Wizara yake kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Centre, Dodoma

 

Dkt. Ndugulile amesema kuwa malengo ya kikao hicho ni kufahamiana, kuwa na mtazamo mpya, uelewa wa pamoja na kujipanga kuendesha Wizara mpya ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara na kudhihirisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa alifanya maamuzi sahihi kuunda Wizara hii

 

Ameongeza kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni njia kuu ya uchumi wa kidijitali kama ilivyo miundombinu mingine ya barabara ambapo taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi wanatumia TEHAMA kuendesha shughuli za kila siku na kuifanya TEHAMA kuchangia ukuaji wa uchumi na kuongeza pato la taifa hivyo taasisi za Wizara zifanye mabadiliko ya kiutendaji, kuboresha sheria, kanuni na miongozo ili kufanikisha utekelezaji wa suala la Tanzania ya uchumi wa kidijitali

 

Amesisitiza kuwa taasisi za Wizara zinazofanya biashara zijiongeze na kuwa wabunifu kwa kufanya utafiti ili kubaini mahitaji ya wateja na kuwafikishia huduma mahali walipo kwa njia ya TEHAMA badala ya wateja kupoteza muda kwa kutafuta ofisi za taasisi ili kupata huduma

 

Aidha, amezitaka taasisi kuandaa mipango mikakati ya taasisi zao ambayo inapimika na inayoenda sambamba na Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, hotuba ya Mhe. Rais Dkt. Magufuli  na Mpango Mkakati wa Wizara ili kuwa na majukumu yanayopimika na utekelezaji wa majukumu kwa matokeo kwa kuwa sio muumini wa michakato

 

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainabu Chaula amesema kuwa Waziri Dkt. Ndugulile ametoa dira na mwelekeo wa kiutendaji kwa Wizara na taasisi zake ili kuhakikisha kuwa Wizara hii mpya inakuwa Wizara ya wananchi kwa kuwa TEHAMA ni ya wananchi

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Dkt. Jones Killimbe amemshukuru Dkt. Ndugulile kwa kuitisha kikao hicho cha kusisitiza utendaji kazi kwa ushirikiano ili kuthibitisha kuundwa kwa Wizara mpya na taasisi ziko tayari kushirikiana ili kufikia malengo yaliyowekwa na Wizara

 

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa taasisi yake imejipanga kutumia teknolojia rahisi ili kufikia malengo ya kufikisha mawasiliano bora na ya uhakika kwa watanzania waishio vijijini

 

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema kuwa Shirika lake litaendelea kuboresha kituo cha huduma kwa wateja kwa kuwa kila siku wanapokea malalamiko ya wateja na wanayashughulikia kwa haraka na TTCL inatumia mitandao ya kijamii na tovuti ili watanzania waweze kupata huduma za TTCL mahali walipo badala ya kwenda kwenye ofisi za TTCL

 

Dkt. Ndugulile amesema kuwa Wizara yake itaendelea kufanya vikao na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zote za Wizara hiyo kila baada ya miezi mitatu ili kupata taarifa, mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu na kujadili taarifa ya mapato na matumizi ya taasisi hizo.

No comments:

Post a Comment

Pages