Naibu
Waziri
wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga katikati akikagua ujenzi wa
chuo cha Veta wilayani Korogwe wakati wa ziara yake kushoto ni Mkuu wa
wilaya ya Korogwe Kissa Gwakisa.
Muonekano wa ujenzi wa baadhi ya majengo ya Chuo cha Veta wilayanu Korogwe.
Fundi akiendelea na ujenzi kwenye Chuo cha Veta wilayani Korogwe kama alivyokutwa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga amefanya ziara ya kutembelea Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wilayani Korogwe Mkoani Tanga huku akitoa wito kwa kamati inayosimamia mradi wa ujenzi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Akiwa katika katika ziara ya kukagua mradi huo ambao unasimamiwa na chuo cha VETA Kihonda cha mkoani Morogoro alionesha kuridhishwa na hatua iliyofikiwa na kushauri matumizi ya jeshi la akiba kama vibarua ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.
Kipanga alisema kwamba amekagua mradi huo na kuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa hadi sasa na kuwaagiza wasimamizi wa mradi kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa ikiwemo kuwashauri kutumia vibarua kutoka Jeshi la Akiba kwa kuwa wapo wengi ambao wanaweza kufanya kazi hizo.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo alitoa wito kwa wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha vifaa vya upauaji vinapatikana mapema ili ujenzi uweze kukamilika kwa muda uliopangwa.
“Kwa kuwa majengo karibu yote yamefikia hatua ya upauaji, nitoe rai kuwa vifaa vya upauaji vipatikane mapema ili ujenzi uendelee na kukamilika kwa wakati,” amesisitiza Mhe. Kipanga.
Awali Akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo hicho, Mkuu wa chuo cha VETA Kihonda, Kashindye Maganga amesema ujenzi wa mradi huo unagharimu kiasi cha Bilioni 1.6 huku kiasi ambacho walikwisha kupokea ni Tsh.Milioni 940.2 na hadi sasa wametumia kiasi cha Tsh.Milioni 917.9 na kiasi kilichobakia ni milioni 22.2 hivyo fedha ambazo imetumika ni sawa na asilimia 57.37 ya fdha ya mradi wote.
Alisema mpaka sasa mradi huo umefikia 34 ya kazi zote na kazi iliyobakia kwa sasa ni kumalizia kufunga lenta,kupaua na kazi ya umaliziaji ambapo tayari walikwisha kuomba fedha kwa ajili ya kumalizia kazi hizo na wanategemea kukamilisha kazi ya mradi huo ifikapo Machi 31 mwaka huu endapo fedha walizoomba watapatiwa mapema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa akizungumza katika ziara hiyo alionyeshwa kufurahishwa na hatua ya Serikali kujenga chuo hicho katika Wilaya yao na kwamba anaamini chuo hicho kikikamilika kitatoa vijana mahiri watakaotumika kiuzalishaji katika viwanda mbalimbali nchini .
No comments:
Post a Comment