Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Zanzibar, Abdalla Duchi (kushoto), akipokea cheti kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mudrik Soraga, ikiwa ni kutambua mchango wa benki hiyo katika kudhamini Tamasha la Saba la Biashara la Zanzibar lililofanyika kuanzia Januari 6 hadi 17. (Na Mpiga Picha Wetu).
Meneja wa benki ya NMB Tawi la Zanzibar, Abdalla Duchi, akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufungwa rasmi Tamasha la 7 la Maonyesho ya Biashara, Maisara mjini Zanzibar.
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mudrik Soraga, amewataka wafanyabiashara kusajili biashara zao hatua itakayowawezesha kutambuliwa rasmi na kuwa walipa kodi ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Alisema hayo alipokuwa akifunga Tamasha la Saba la Biashara la Zanzibar kwenye viwanja vya Maisara Jijini Zanzibar, tamasha ambalo hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kusherehekea Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo kwa mwaka huu yametimiza miaka 57.
Soraga aliwasihi wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kushiriki matamasha mbalimbali ya biashara ya ndani na nje ili kuwaongezea uzoefu hatua itakayowawezesha kupanua wigo wa soko la bidhaa zao na kujiongezea kipato wao binafsi na taifa kwa ujumla.
“Tuna adhma ya kuwaalika wafanyabiashara wa mataifa mengine kushiriki tamasha hili katika miaka ijayo hatua itakayolifanya kuwa la kimataifa na kuongeza wigo kwa wafanyabiashara wa ndani kujifunza zaidi” alisema Soraga.
Aidha katika hafla hiyo, Soraga alikabidhi tuzo kwa Benki ya NMB na taasisi kadhaa ambazo zilidhamini Tamasha hilo la Saba la Biashara la Zanzibar.
Akizungumza baada ya kupokea Tuzo, Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Zanzibar, Abdalla Duchi, alisema kuwa benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora zaidi kwa lengo kukidhi mahitaji ya wateja wake ili kwenda sanjari na sera ya Zanzibar ya uchumi wa Buluu.
“Benki yetu ni wadau wakuu wa viwanda na wafanyabiashara wadogo wadogo hivyo ili kuboresha mustakabali wao tunalazimika kuwa na huduma bora zaidi kwa wateja na hata taasisi hususani za kijamii” Alisema Duchi.
Pamoja na hayo, aliishukuru Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kwa kuandaa Tamasha hilo kwa kuwa limetoa fursa kwao (NMB) kujifunza zaidi pamoja na kupata wigo mzuri wa kuonesha huduma zao.
Tamasha la Biashara la Saba la Zanzibar lilikuwa na washiriki 360 ambalo ilifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Januari 6 na lilifungwa Januari 17 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment