Talib Ussi, Zanzibar
Mwenyekiti wa Chama cha ADC Hamad Rashid Mohamed amesema wanaume wengi wamekua wakishindwa kuwaunga mkono wake zao katika harakati za uongozi kufuatia hofu ya kuvunjika ndoa zao.
Alisema licha ya uwepo wa muamko mkubwa kwa wanawake Zanzibar lakini bado wanawake wengi hushindwa kufikia malengo yao kwa kile anachokiona ni kukosa hamasa kutoka kwa watu wa karibu.
Hamadi ambae pia ni Waziri mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar awamu ya saba aliyasema hayo wakati alipokua akichangia uwasilishwaji wa rasimu mpya ya kuwawezesha wanawake wa Zanzibar kushika nafasi mbalimbali za uongozi hafla iliofanyika katika ukumbi wa Tamwa Tunguu Wilaya ya kati Unguja.
Amesema ipo haja kwa wanaume walio kwenye ndoa kujitathmini na kukubaliana na maamuzi ya wake zao wakiamini kuwa mwanamke kuwa kiongozi si sababu ya kuvunjika kwa ndoa.
‘’Wapo wanawake wengi ambao wanatunza na kulinda ndoa zao licha ya kuwa ni viongozi hivyo ni mtu tu mwenyewe kujitambua kwa kuwa wapo wanawake na wanaume viongozi na wanaheshimu ndoa zao’’aliongezea.
Awali akiwasilisha rasimu yenye lengo la kuwainua wanawake Zanzibar katika nafasi za uongoizi Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Dkt,Salum Sleiman Ally alisema licha ya jitihada mbali mbali zinazoendelea kufanyika lakini bado wanawake wengi wapo nyuma katika nafasi za uongozi Znzibar.
Alisema katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar wapo wanawake wengi wenye uwezo mkubwa wa kuwa viongozi iwapo wangepewa nafasi kwenye jamii zao.
Hata hivyo Mhadhiri huyo alieleza kuwa kuna haja ya mabadiliko makubwa kwenye jamii na vyama vya siasa mabadiliko ambayo yataweka wazi ikiwezekana hata kuandikwa kwenye katiba za vyama vyote vya siasa.
Kwa upande wake Dkt,Mohamed Said Dimwa alisema Zanzibar imekua na idadi kubwa ya wapiga kura wanawake kuliko wanaume lakini cha kushangaza wanawake wamekua wakikosa fursa za kuchaguliwa.
Alisema jamii ya wanawake wanapaswa kubadili mitazamo yao na kuona kuwa wanawake wenzao wanaweza kuwa viongozi na sio kuwadharau na kuona kuwa hawawezi kufanya lolote lile.
‘’Mimi binafsi mke wangu aliingia kwenye kinyanganyiro cha Urais kupitia chama cha Mapinduzi CCM na nilikua wa kwanza kumuunga mkono kwa kuwa najua umuhimu wa wanawake kwenye uongozi’’aliongezea.
Sambamba na hayo Dimwa aliongezea na kueleza kuwa ipo haja ya vyama vya siasa kuwa na uwazi kwenye nafasi mbali mbali za uongozi ili walio wengi waweze kushiriki na kuamini maamuzi yanayofanywa na vyama husika.
Nae Bi Janeth Fussi ambae ni Katibu Mtendaji Taifa kupitia Ngome ya wanawake Chama cha ACT Wazalendo alisema katika changuzi mbali mbali zimekua na pirika zake lakini wanawake wanaogombea hukosa ulinzi stahiki kama wagombea.
Alisema inasikitisha sana kuona waliopewa mamlaka ya ulinzi kuwa ndio wanakua mstari wa mbele kuwadhalilisha wanawake wanaogombea kupitia nafasi mbali mbali za uongozi.
‘’Ipo haja elimu hii kuendelea kutolewa zaidi katika jamii na vyombo husika ikiwemo kutambuliwa utu wa mwanamke kwenye jamii na vyombo husika.
Mradi wa uwezeshaji wanawake katika nafasi za uongozi kwa kila wilaya Zanzibar ni wa miaka mine kutoka mwaka mwaka 2020 -2023 na utatekelezwa na Tamwa-Zanzibar,Zafela pamoja na Pegao chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway Tanzania.
No comments:
Post a Comment