Nyavu haramu 1565 zenye thamani ya Sh. Bilioni 1.4 zikiteketezwa mkoani Kagera.
Na Lydia Lugakila, Muleba
Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Muleba mkoani Kagera imefanikiwa kuteketeza nyavu haramu zipatazo 1565 zenye thamani ya bilioni 1.4 katika mwaro wa magarini uliopo katika kata ya Nyakabango.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Wilayani humo ambaye pia ni mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Ruyango nyavu hizo zipo zilizo salimishwa na nyingine kukamatwa katika zoezi la doria iliyoendeshwa kwa kipindi cha mwaka 2019/2020.
Mhandisi Ruyango amesema kuwa nyavu hizo zilizokamatwa na kusalimishwa ni kokoro 538, nyavu ndogo za dagaa 12, timba 305, nyavu ndogo za makila 705 na katuli 5 .
Kufuatia Hali hiyo kamati hiyo imesema haitomfumbia macho mvuvi yoyote ambaye atavua kinyume na sheria katika ziwa victoria.
Kwa upande wake Afisa Uvuvi Wilaya ya Muleba, Wilfred Tibendelana, amesema katika kuendelea kudhibiti uvuvi usiokubalika kisheria huku halmashauri hiyo ikiahidi kuendelea kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa vijiji na kata ili kulinda rasilimali za ziwa victoria na Burigi.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wilayani Muleba wameshukuru kamati hiyo kwa zoezi hilo licha ya uwepo wa changamoto ya baadhi ya viongozi waliopo katika maeneo yao kujihusisha na vitendo vya rushwa baina yao na wavuvi hivyo kuishauri ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kufanya doria za mara kwa mara ili kuwachukulia hatua Kali za kisheria viongozi hao.
No comments:
Post a Comment