HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 09, 2021

TASAF YABORESHA MAISHA YA WANANCHI KIJIJI CHA BWITI

Na James Mwanamyoto-Mkinga

  

Wananchi wanaoishi katika kaya maskini Kijiji cha Bwiti, wilayani Mkinga wanaonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wamewezeshwa kuboresha makazi yao, kufanya shughuli za ufugaji, ujasiliamali, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii, kujishughulisha na kilimo ikiwa ni pamoja na kumudu
gharama za mahitaji ya shule kwa watoto wao.


Wananchi hao wametoa shuhuda za mafanikio waliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Tanga.


Mmoja wa wanufaika Bi. Fatuma Mohamed Hamza amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, ruzuku aliyoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imemuwezesha kununua bati 40 alizoziezeka katika nyumba yake na hatimaye kuondokana na adha ya kunyeshewa na mvua aliyokuwa akikabiliana nayo kwa kipindi kirefu.


Naye, mjane Bi. Mwajuma Ayubu Bakari amesema, baada ya kupokea ruzuku yake kwa vipindi vitatu mfululizo aliwekeza kidogo kidogo na hatimaye kuweza nununua mbuzi ambapo mpaka hivi sasa amefanikiwa kuwa na mbuzi wapatao 14 na kuongeza kuwa, ruzuku pia inamuwezesha kugharamia mahitaji ya watoto shuleni.


Mnufaika mwingine, Bi. Mwajuma Said Kidevu amemthibitishia Mhe. Ndejembi kuwa, kabla ya kupokea ruzuku alikuwa na mbuzi 6 lakini baada ya kuanza kupokea ruzuku ameweza kuongeza idadi ya mbuzi anaowafuga hadi kufikia 12.


Akizungumzia mafanikio aliyoyapata, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, kupitia ruzuku anayoipata ameweza kujenga nyumba bora yenye choo bora, anajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na ameweka umeme nyumbani kwake, hivyo anaishukuru Serikali kwa kuanzisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao kwa kiasi kikubwa umeboresha maisha yake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi mara baada ya kupokea shuhuda hizo, amewataka walengwa wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kutumia vema ruzuku wanazozipata kujikwamua katika umaskini ili kutimiza lengo la Serikali kuwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Ndejembi amesisitiza kuwa, matumizi mazuri ya ruzuku ni sehemu ya kuunga mkono azma ya Mhe. Rais ya kuuendeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kuboresha maisha ya wanyonge nchini.
 

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka waratibu wa TASAF nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya namna bora ya kutumia ruzuku wanazopatiwa walengwa wa TASAF na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha ruzuku wanazopatiwa zinatumika kuboresha maisha yao na kuweza kuhitimu kwa lengo la kutoa fursa kwa kaya nyingine kunufaika na
ruzuku inayotolewa na TASAF.

No comments:

Post a Comment

Pages