HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 03, 2021

WATENDAJI WA TANESCO NA REA WAPEWA MAAGIZO

NA DANSON KAIJAGE, MWANZA 


Waziri wa Nishati, Mhe. Dk Medard Kalemani, amewaagiza watendaji wa TANESCO na REA, kuhakikisha wanawaunganishia umeme wateja wote waliolipia ankara za umeme jijini Mwanza na maeneo ya vijijini ndani ya miezi mitatu kuanzia mwishoni mwa mwaka jana.

Waziri Kalemani ameyasema hayo, alipokuwa akizungumza na Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kikao kazi cha pamoja kilichofanyika kwenye ukumbi wa  Benki Kuu jijini Mwanza.

Waziri Kalemani, amewaelekeza watendaji hao wa TANESCO  kuhakikisha wateja wote walioko katika maeneo ya vijijini na kando kando ya miji, wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000 bila kujali umbali wa mita 30 kwani ni wajibu wa TANESCO kuwafikishia wananchi nguzo za umeme ili kuwafikia wateja hao. 

"Mnataka kila mwananchi awe mita 30 ndipo muwafikishie umeme? Ni kazi yenu kupeleka nguzo hadi muwafikie wananchi hao. Nimeambiwa mnasubiri sekula hii sasa ndiyo sekula na wapa. Ni sisikie mtu anaongelea suala la mita 30 amesema Kalemani."

Waziri Kalemani, ameitaka TANESCO  kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja ili kuhakikisha wateja wanapatiwa huduma bora na kwa wakati na kuwaondolea adha ya kufuatilia maombi ya kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi  za TANESCO Wilayani.

Amewataka watendaji wa TANESCO kuwafuata wateja mahali walipo na kuepuka kutumia lugha ya kukatisha tamaa kwa wateja ili kujenga mahusiano mazuri na wateja  jambo litakalopelekea kupanua wigo wa wateja na kuongeza mapato kwa Shirika.

" Masurveyor ndio wanaolalamikiwa sana kwa kutoa lugha zinazokatisha tamaa. Ninawasihi mbadilike kuanzia sasa. Atakayebainika anatumia lugha mbaya kwa mteja, huyo tutaachana nae na atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Wateja wote wahudumiwe bila kubaguliwa. Tunataka wateja wote wapate umeme bila kubaguliwa. Amesema Dkt. Kalemani.

Aidha,  Dkt. Kalemani, amewapongeza watumishi wa TANESCO kwa utendaji mzuri na kueleza kuwa kwa zaidi ya asilimia 80 utendaji wa TANESCO ni wa Kuridhisha.

Waziri Kalemani amesifu utendaji mzuri wa Meneja wa TANESCO Kanda ya Ziwa Mhandisi Henryfried Byabato na kueleza kuwa utendaji mzuri wa kazi katika maeneo mengi aliyofanya kazi ndiyo uliopelekea Mha. Byabato kupandishwa cheo.

Waziri Kalemani pia ameelekeza watumishi walioajiriwa kwa muda (Short Term Employees - STE) wanaohusika na kazi za kuwapimia umeme wananchi wanunuliwe pikipiki zitakazowawezesha kuwafikia wateja kwa urahisi. 

Aidha, ameagiza kuwa watumishi hao (STE) wanaofanya kazi vizuri na waliofanya kazi kwa muda mrefu waombewe kibali cha ajira ya kudumu Utumishi kupitia Wizara ya Nishati.

Waziri Kalemani amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na kwa usahihi na amewataka watumishi wa TANESCO na REA kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi hicho, Naibu Waziri Byabato, amewataka watumishi wote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Kalemani, na atahakikisha anasimamia na kufuatilia utekelezaji wake kwa ukamilifu.

Kikao kazi baina ya Waziri  Kalemani na watumishi wa TANESCO na REA, ni kikao kazi cha pili baada ya kikao na wafanyakazi wa Mkoa wa Geita wiki moja iliyopita. Lengo la vikao hivyo ni kuweka misingi ya pamoja ya utendaji kazi unaolenga kuleta matokeo chanya na ya haraka katika Sekta ya Nishati.


No comments:

Post a Comment

Pages