WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameshiriki mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia (CCM) mkoa wa Manyara Martha Umbulla na ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wamuezi kwa kuayaendeleza mambo mema ayaliyofanya katika kipindi cha uhai wake.
Mazishi hayo ya Martha yamefanyika leo (Jumanne, Januari 26, 2021) nyumbani kwake katika kijiji cha Dongobesh wilayani Mbulu mkoa wa Manyara. Mbunge huyo alifariki Jumanne, Januari 21, 2021 katika Hospitali ya HCG Mumbai, India alikokuwa anatibiwa.
“Nimekuja kuungana nanyi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa mume wa marehemu, watoto na familia kufuatia msiba mzito wa kuondokewa na mpendwa wetu Mheshimiwa Umbulla.”
Waziri Mkuu amesema tukio hilo ni zito na ni ngumu kuishi nalo kwa sababu marehemu Martha aliishi vizuri na wabunge wenzake na pia katika kipindi chote cha ubunge wake aliishauri vizuri Serikali. “Kifo chake ni pigo kubwa kwa Serikali, hivyo itaendelea kuthamini na kuuenzi mchango mkubwa alioutoa.”
Amesema jambo la muhimu kwa sasa ni kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema. “Mume wa marehemu, watoto, ndugu, jamaa, wabunge na wananchi wa Mkoa wa Manyara namuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”
No comments:
Post a Comment