Wakulima wa Misiti ya Misaji (Teak) kutoka kijiji cha Mkali A
wakishiriki kupanda miti hiyo kibiashara katika shamba la moja wapo.
Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda akieleza waandishi wa habari ni sababu gani imewasukuma kubuni program hiyo.
Ofisa Misitu na Mratibu wa FORVAC Wilaya ya Nyasa, Bugingo Bugingo
akitoa maelezo kuhusu faida za Miti ya Misaji (Teak), ambayo inapandwa
katika vijiji vya Liuli, Lipingo, Mkali A na Mkali B wilayani hapo.
Muonekano wa Miti ya Misaji (Teak) ambayo imepandwa katika mashamba mbalimbali ya wakulima wa vijiji vya Liuli, na Mkali A.
NA SULEIMAN MSUYA, NYASA
SHUGHULI za upandaji miti kibiashara ambazo
zinafadhiliwa na Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu
(FORVAC) katika vijiji vinne vya Liuli, Lipingo, Mkali A na Mkali B
inatarajiwa kuzalisha mamilionea 599 wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
FORVAC
inatekelezwa na Idara ya Misitu na Nyuki kwa kushirikiana na Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Program
inatekelezwa katika Kongani tatu za Tanga (Handeni, Kilindi, Mpwapwa na
Kiteto); Kongani ya Lindi (Wilaya za Liwale, Ruangwa na Nachingwea) na
Kongani ya Ruvuma (katika Wilaya za Tunduru, Namtumbo, Songea, Mbinga na
Nyasa) na inafadhiliwa na Serikali mbili za Tanzania na Finland.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hii Mwenyekiti wa Chama cha Wapandaji Miti
Kibiashara (TGA) Kata ya Liuli Samwel Mawanja, amesema program ya FORVAC
ambayo inawapa fursa ya kupanda miti imeanza kuleta matumaini makubwa.
Mawanja
amesema katika kata ya Liuli vijiji vinne ambavyo vipo kwenye program
ya FORVAC zaidi ya wanavijiji 500 wamepanda miti ya Misaji (Teak) ambapo
baada ya miaka 20 watavuna na kuanza kuuza.
Mwenyekiti
huyo amesema mwitikio wa wananchi wa vijiji hivyo vya Lipingo, Liuli,
Mkali A na Mkali B kupanda miti umekuwa mkubwa hasa baada ya kupata
elimu hali ambayo inavutia wengine.
"Tumeamua
kushiriki katika mradi huu baada ya kupata elimu ya faida ya Misaji.
Hadi sasa tupo zaidi ya 500 ambapo kila mmoja ana hekari mbili za
kupanda hivyo zaidi ya hekari 1,000 zimepandwa misaji na hekari moja
inaweza kumpatia mkulima zaidi ya shilingi milioni 300 baada ya miaka
20," amesema Mawanja.
Mwenyekiti
huyo amesema kwa sasa kuna wakulima 599 ambapo kijiji cha Liuli kina
wakulima 296 wa Miti ya Misaji, Lipingo zaidi 150, Mkali A 116 na Mkali B
37 ila wanatarajia wataongezeka kwa kuwa elimu imeendelea kutolewa.
Amesema wanashuruku FORVAC kuwawezesha mbegu ya Misaji na kuahidi kuwa watahakikisha hawawaangushi.
Mwenyekiti
wa TGA ya Mkali B, Magreth Ngonyani, amesema ujio wa program hiyo
umefungua kurasa mpya ya maisha yao kwani wanaamini miaka michache ijayo
watatambulika kama mamilionea.
Ngonyani
amesema wanashiriki program hiyo wakiwa na amani kwa kuwa haiwabani
kufanya shughuli nyingine za uzalishaji huku wakiwa na matumaini ya
kunufaika.
"Sisi hapa
tumeelimishwa na wataalam wa FORVAC na Serikali kuhusu faida ya miti ya
Misaji hivyo tuna imani kuwa siku chache tutabadilishwa majina kwa
kuitwa mamilionea," amesema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa TGA ya Mkali A, Alphonce Sangana amesema
wanakijiji wamepokea program hiyo kwa moyo wote jambo ambalo
linarahisisha utekelezaji na usimamizi wake.
Sangana
amesema wamepanda miche zaidi 50,000 kwenye hekari zaidi ya 100 hivyo
matumaini yao ni kuwa baada ya miaka 20 watakuwa na mamilionea wengi.
Mwenyekiti
huyo ambaye pia Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema
program hiyo imeanza kuonesha matumaini ila changamoto kubwa ni
kukosekana miundombinu ya uhakika ya kuwafikisha shambani.
"FORVAC
imekuja kutekeleza Ilani ya CCM, inayotaka mazao ya misitu kuongezewa
thamani mimi nikiwa muenezi nitaendelea kupigania hili kwa nguvu zote,"
amesema.
Menedora Haule
Mwekahazina wa TGA ya Mkali A, amesema yeye amefanikiwa kupanda miche
520 ambapo anaamini siku chache zijazo zitabadilisha maisha yake.
Haule amesema amekuwa akitoa elimu kwa wakina mama wenzake ili washiriki program hiyo kwa kuwa itabadilisha maisha yao.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Mkali A, Barnabas Mbele amesema program hiyo ya FORVAC ni
mkombozi wa wanakijiji na kuwa watakuwa bega kwa bega kuhakikisha
inafanikiwa.
Amesema program hiyo imeweza kuajiri vijana wengi kijiji kwake hivyo hawana budi kuiunga mkono ili iwe endelevu.
"Mimi
kama Mwenyekiti wa kijiji ninayetokana na CCM nadiriki kusema program
ya FORVAC inatekeleza Ilani ya chama hivyo tutaiunga mkono bila shaka,"
amesema.
Kwa upande wake
Ofisa Misitu na Mratibu wa FORVAC Wilaya ya Nyasa Bugingo Bugingo,
amesema program hiyo itakuwa na matokeo chanya kwa wanavijiji siku
chache zijazo.
"Nikizungumza
kama mtaalam niseme kuwa baada ya miaka 20 hapa Liuli kutakuwa na
mamilionea wengi ambao watatokana na kilimo cha Misaji.
Kwa
mujibu wa taarifa za sasa ujazo wa mita moja ya Mti wa Msaji unauzwa
hadi shilingi laki 8 hivyo kwa mtu mwenye miti 350 akivuna kwa pamoja
anaweza pata zaidi ya shilingi milioni 350 kwa hekari moja," amesema.
Amesema Misaji ni miti ambayo inatumika kutengeneza vya thamani kama meli, jahazi na vitu vingine.
Bugingo amewashauri wanavijiji kuhamasishana kupanda miti ya Misaji kwa kuwa ni fursa kubwa ya kiuchumi.
Mratibu
wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda amesema wametoa miche ya
Misaji 450,000 ambayo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 225 lengo
likiwa ni kuinua maisha ya wanavijiji nakuonesha kwa vitendo dhana nzima
ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu.
Mutunda
amesema FORVAC inaaamini iwapo kila mwanakijiji atatambua dhana ya
mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu ni wazi kuwa wataitunza na
kuilinda misitu.
"Sisi
tunataka Tanzania iwe na mamilionea wengi kupitia rasilimali zao na
misitu ni moja wapo hivyo tutatoa ushirikiano na yoyote ambaye ataonesha
kuhitaji," amesema.
Mkuu
wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chillumba amesema wao kama wilaya wataungana
na mdau yeyote ambaye atakuwa amekuwa na wazo la kumkomboa mwananchi
kiuchumi, maendeleo na huduma za kijamii.
Aidha,
amesema wilaya kupitia Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA),
watajitahidi kutatua changamoto ya miundombinu katika vijiji vyote ili
shughuli za maendeleo zitekelezwe.
"Tunawakaribisha wadau wote ambao wana mitazamo kama ya FORVAC ili kuchochea maendeleo wilayani kwetu," amesema.
No comments:
Post a Comment