Wanafunzi
wa Shule ya Msingi Nambila kijiji cha Mkali A Kata ya Liuli wilayani
Nyasa mkoani Ruvuma wakivuka Mto Mbahwa hali ambayo ni hatari kwa maisha
yao.
Mkazi wa Kijiji
cha Mkali B, Kata ya Liuli mkoani Ruvuma, John Nombo akielezea namna Mto
Mbahwa ulivyo kero kwa wanafunzi na wananchi wa kijiji hicho.
NA SULEIMAN MSUYA, NYASA
KUKOSEKANA
kwa daraja la uhakika Mto Mbahwa katika vijiji vya Mkali A na Mkali B,
Kata ya Liuli wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, kumetajwa kuhatarisha
usalama na maisha ya wanafunzi na wananchi wa vijiji hivyo.
Mwandishi
wa habari hii alitembelea mto huo hivi karibuni ambapo alishuhudia
wanafunzi na wananchi wanaoishi maeneo ya mashambani wakivuka kwa shinda
baada daraja la awali kusombwa na maji.
Akizungumzia
adha hiyo Mwanafunzi Neema Kawonga wa Shule ya Msingi Nambila, amesema
kukosekana kwa daraja hilo kunahatarisha maisha yao na mahudhurio kuwa
hafifu.
Mwanafunzi huyo
amesema wamekuwa na moyo wa kusoma ila changamoto ya Daraja la Mbila
inawakatisha tamaa hivyo wanaiomba Serikali iwasaidie kujenga.
Kawonga amesema kutokana na kero hiyo hasa kipindi cha masika kama sasa wanashindwa kwenda shule kwa kushindwa kuvuka maji.
"Tunapenda
shule pamoja na umbali wa zaidi ya kilometa tatu ila tukifika hapa
darajani maji yamejaa tunarudi nyumbani inauma sana," amesema.
Kawonga
amesema kutokana na changamoto hiyo wapo wanafunzi wanaokata tamaa ya
kusoma hivyo ombi lake ni serikali kujenga daraja katika eneo hilo.
"Huku
ndipo wanazaliwa waandishi, wahandisi, walimu, madaktari, wahasibu na
wengine tunaomba Serikali au wadau wajitokeze kutujengea daraja hili
muhimu," amesema.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule Nambila Erasimus Haule amesema
kukosekana kwa daraja hilo kuna madhara makubwa kwa wanafunzi wanoishi
upande wa mashambani.
Haule amesema wanafunzi wamekuwa wakikosa vipindi wakati wa masika jambo ambalo linashusha ufaulu wao.
"Ni
kweli kukosekana kwa daraja kuna athari kubwa kwa wanafunzi wangu zaidi
150 wanaishi upande wa mashambani naomba Serikali ifanyie kazi hii
changamoto," amesema.
Naye John Nombo Mkazi wa Kijiji cha Mkali B amesema ukosefu wa daraja sio changamoto kwa watoto pekee hata kwa wananchi wengine.
Nombo amesema wakati wa mvua za masika hata watu wazima wanashindwa kwenda mashambani na wamashambani wanashindwa kuja mjini.
"Hapa
tatizo ni kubwa sana sio kwa watoto wa shule pekee hata sisi watu
wazima kipindi cha masika hatufanyi kazi za kilimo na ukikutwa na mvua
shambani basi inabidi ubaki huko hadi mvua iishe," amesema.
Mbunge
wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya amesema changamoto hiyo
miumbombinu anaijua na amekuwa akiiombea hela mara kwa mara.
Amesema Halmashauri imekuwa ikitafuta fedha za kujenga daraja katika eneo hilo ili kuondoa adha hiyo kwa wanafunzi na wananchi.
"Changamoto
hiyo inajulikana na tumekuwa tukiiombea fedha kuanzia ngazi ya
halmashauri na bungeni ila bajeti inayotolewa kwa Wakala wa Barabara
Mijini na Vijijini (TARURA) ni ndogo," amesema.
Mhandisi
Manyanya amesema jimbo hilo lina changamoto ya miundombinu hivyo
kuwaomba wapiga kura wake na subira kwani Serikali inafanyia kazi.
Akizungumzia
kadhia hiyo Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chillumba amesema Serikali
inatambua changamoto za miundombinu ya daraja katika vijiji vya Mkali,
A, B na Liuli hivyo watajitahidi kurekebisha.
Chilumba
amesema Serikali ya wilaya inaendelea kutafuta fedha kupitia vyanzo
vyake mbalimbali ili kuhakikisha miundombinu yote inakuwa salama na
kupitika muda wote.
"Miundombinu katika wilaya yetu kwa baadhi ya maeneo ni changamoto hivyo tunapambana kuipatia ufumbuzi," amesema.
No comments:
Post a Comment