Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu Mpya wa Wizara yake ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba (wa tatu kulia) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Adolf Ndunguru (kushoto) pamoja na Karani wa Baraza la Mawaziri Nsubili Joshua.
NA BENNY MWAIPAJA, DAR
WAZIRI
wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba, amewahakikishia wafanyabiashara
hapa nchini kuwa Wizara yake itahakikisha inarejesha taswira na
mahusiano mazuri nao katika masuala yakodi ili kuboresha mazingira ya
ufanyaji biashara na kusisimua uchumi wa nchi.
Dk. Nchemba alitoa
ahadi hiyo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipozungumza na vyombo vya
habari baada ya tukio la kuapishwa kwa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu
Wakuu pamoja na viongozi wa Taasisi, tukio lililofanywa na Rais Samia
Suluhu Hassan.
“Tutatengeneza vyanzo vipya vya makusanyo ili
mzigo wa kodi usibebwe na wachache kwa sababu kadri mzigo unavyobebwa na
wengi ndivyo nafuu inavyopatikana, hatua itakayowafanya wafanyabiashara
wengi kulipa kodi kwa hiari” alieleza.
Aidha, Dk. Nchemba
aliyeanza kazi hivi karibuni kama Waziri wa Fedha na Mipango, alisema
kuwa amekutana na wataalam wa Wizara yake na kuwaagiza wakutane na
wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kujadili namna ya kutatua
changamoto za Muungano na kwamba anaamini zitapatiwa ufumbuzi.
“Shida
ya watu wetu wengi wanapojadili masuala haya hawatuambii walipokwama,
kwahiyo niliwaambia watubainishie wanapokwama ili tupate ufumbuzi wa
jambo hilo baada ya hapo tutakaa Wizara tatu, Wizara ya Fedha na
Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais
na kufanya uchambuzi wa kina” Alifafanua Dk. Nchemba.
Kuhusu
udhibiti wa matumizi wa Fedha za Umma, Dk. Mwigulu alisema kuwa Wizara
yake itatumia mifumo ya fedha iliyobuniwa kudhibiti matumizi ya Serikali
na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili iwe michache lakini
yenye ufanisi pamoja na kuimarisha masuala ya utawala katika kukusanya
mapato na matumizi yake ili fedha hizo zilete matokeo yaliyokusudiwa.
Waziri
huyo alishuhudia kuapishwa kwa watendaji wake wapya, akiwemo Katibu
Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali Emmanuel Tutuba na Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Dk. Khatibu Kazungu ambao wameapishwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Ikulu, jana Jijini Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment