JOWUTA imepokea kwa furaha, faraja na matumaini makubwa maelekezo hayo ambayo yatasaidia kundi kubwa la vijana waandishi wa habari ambao walikosa kazi baada ya vyombo vyao kufungiwa.
JOWUTA inaamini kuwa uamuzi huo wa Mheshimiwa Rais wa kutolewa vifungoni kwa vyomvo hivyo, utasaidia kurejesha na kuongeza ajira kwa kundi kubwa la vijana ambalo liliathirika na ufungaji huo.
Aidha, JOWUTA inaamini kurejeshwa kwa vyombo hivyo Serikali itaweza kukusanya kodi ambayo itatumika kutekeleza miradi mbalimbali muihimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Pia, JOWUTA inamwomba Mheshimiwa Rais kusaidia kufutwa kwa sheria kandamizi zinazotumika kuadhibu vyombo vya habari nchini na pia kuweka mazingira bora ya kuvisaidia vyombo vya habari na wana habari kuteleza wajibu wao kwa haki,usawa na bila ubaguzi wa aina yoyote.
“Vyombo vya Habari viwe vya serikali au binafsi vina dhima moja kubwa ya kuitumikia jamii. Utamaduni ulioanza kujengeka wa kubagua vyombo vya habari kwa misingi yoyote ile, unatugawa na lazima sote tuungane kupiga vita kansa hii inayotutafuna taratibu,”ilisisitiza sehemu ya taarifa hiyo
JOWUTA kikiwa chombo muhimu na kiunganishi kati ya vyombo vya habari na Serikali, inaahidi kushirikiana na wadau wengine wa habari kuhakikisha maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa yanatekelezwa ili kuhakikisha tasnia ya habari inafuata weledi, kanuni na sheria za nchi.
Kwa upande mwingine JOWUTA inaviomba vyombo vya habari na wana habari nchini kutekeleza majukumu yao muhimu kwa taifa wakiongozwa na uzalendo na kufuata misingi ya uandishi wa habari, sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“JOWUTA inaamini iwapo vyombo vya habari vitazingatia na kufuata misngi, maadili, kanuni na sheria za habari vitakuwa vinatimiza wajibu wao muhimu kwa nchi yetu”
JOWUTA inampongeza Rais Samia kwa kutoa hotuba nzuri na yenye kuleta matumaini kwa Watanzania wote na kuahidi kuunga mkono Serikali katika azma yake ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment