Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Andrew Massawe (kushoto) akisaini hati za makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) jana Jijini Dodoma. (Picha na Wizara ya Kilimo).
Aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) akikabidhi nyaraka na taarifa mbalimbali kwa Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Kilimo Bw. Andrew Massawe (kushoto) Jijini Dodoma. Kwa sasa Kusaya ameteuliwa kuwa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof. Siza Tumbo (aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi baina ya Katibu Mkuu Bw. Andrew Massawe (katikati) na aliyekuwa Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia).
Na Mwandishi Wetu
Aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ambaye sasa ni Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya jana amekabidhi rasmi ofisi kwa Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Kilimo Bw. Andrew Massawe halfa iliyofanyika Dodoma kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan hapo April 04 mwaka huu.
Akizungumza kwenye kikao kilichohudhuriwa na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo jana (14.04.2021) Kamishna Jenerali Kusaya alisema serikali ya Awamu ya Sita imepanga kuona kilimo kinakuwa na mchango mkubwa kwenye upatikanaji ajira na kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi.
"Kilimo ni ajira,kilimo ni biashara hivyo wakulima waendelee kujikita kwa bidii huku wakizingatia matumizi ya kanuni bora za kilimo na matumizi ya mbegu na pembejeo za Bora" alisisitiza Kusaya.
Kuhusu mapambano ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Kamishna Jenerali Kusaya ametoa wito kwa wakulima na wananchi kushirikiana na serikali kwa kuwafichua wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo bangi na mirungi ambayo inaathiri maisha ya vijana ambao ni nguvu kazi .
Kusaya alisema " tujione kuwa tuko ndani ya vita,tubebe silaha ili kudhibiti dawa za kulevya ambazo zinaathiri vijana wenye nguvu za kutenda kazi " na kuwa Mamlaka yake imedhamiria kuona biashara hii haramu inadhibitiwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu mpya Wizara ya Kilimo Bw. Andrew Massawe alisema atahakikisha kazi zilizopangwa ikiwemo miradi ya kuwezesha wakulima kunufaika na kilimo inatekelezwa kwa ufanisi .
Massawe ameongeza kusema kipaumbele chake ni kuona Wizara ya Kilimo ikipeleka teknolojia ya kisasa kwenye uzalishaji wa mazao ya wakulima ikiwemo mifumo ya kurahisha utatuzi wa kero .
"Wizara hii ni inabeba kundi kubwa la Watanzania ambapo kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi hivyo nitahakikisha elimu inawafikia wakulima waongeze uzalishaji na tija kwenye kilimo" alisema Massawe.
Kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Kilimo Katibu Mkuu Massawe alikuwa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayaeshughulikia Ajira,Vijana na Kazi.
No comments:
Post a Comment