Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera inamshikilia
mkufunzi mmoja aliyetambulika kwa jina la Ruta Cleophace Kyaragaine
mwenye umri wa miaka 59 kwa tuhuma za kumuomba rushwa ya ngono
mwanafunzi.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Mkuu wa
Takukuru mkoani Kagera, John Joseph (pichani), amesema mkufunzi huyo
anashikiliwa kufuatia kupokewa kwa taarifa kutoka kwa mwanafunzi mmoja
ambaye anasoma katika chuo hicho (jina lake kozi anayosoma
vimehifadhiwa) kuwa mkufunzi huyo aliyejulikana kwa majina ya Ruta
Cleophace Kyaragaine amekuwa akimuomba rushwa ya ngono mwanafunzi huyo
tangu mwaka 2020 kwa madai ya kwamba atamsaidia ki masomo na kuwa endapo
hatokubali kushiriki naye ki ngono basi hatomaliza masomo yake.
John
Joseph amesema kuwa kufuatia kupokewa kwa taarifa hiyo taasisi hiyo
ilianza uchunguzi mara moja ambapo Aprili 3, 2021 maafisa hao
walimkamata mkufunzi huyo katika nyumba ya kulala wageni iliyopo
Manispaa ya Bukoba Mkoani humo akiwa na mwanafunzi huyo huku
akilazimisha kupewa ngono na kutoa baadhi ya ahadi na vitisho kwa
mwanafunzi huyo.
"Uchunguzi wa tuhuma hii uko katika hatua za
mwisho na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili aweze kujibu
tuhuma hizo zinazomkabili" alisema Joseph.
Hata hivyo mkuu huyo
wa Takukuru ametoa wito kwa wananchi Mkoani humo kutambua kwamba rushwa
ya ngono ni rushwa inayotakiwa kupingwa kwa nguvu zote kwani
hudhalilisha utu wa mwanamke na madhara yake ni makubwa mno.
No comments:
Post a Comment