HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 10, 2021

WAZIRI WA KILIMO PROF. MKENDA AMUOMBA BALOZI WA UHOLANZI WAWEKEZAJI ZAIDI KWENYE KILIMO

 

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda, akizungumza na mgeni wake Balozi wa Uholanzi nchini Jeroen Verheul ofisini kwake Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.


Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda Aprili 9, 2021 amekutana na Balozi wa Uholanzi nchi Jeroen Verheul na kumwambia Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji katika Sekta ya Kilimo na kumuomba kushawishi uwekezaji kwenye Sekta ya Kilimo hususan kwenye uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta, usindikaji wa mafuta ya kula, uzalishji wa mazao ya mboga, matunda, viungo,maua pamoja na upatikanaji masoko ya mazao hayo.

“Nafikisha ombi kwako la kutusaidia kushawishi Wawekezaji zaidi nchini kwenye eneo la uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta, usindikaji wa mafuta ya kula na usindikaji wa mazao ya aina mbalimbali kwenye Sekta ya Kilimo pamoja na masoko ya mzao hayo.” Amesisitiza Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda amesema Wizara ya Kilimo imejipanga ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo inachangia ukuaji wa uchumi kwa kuongeza mara dufu fedha katika eneo la utafiti wa mazao ya mbegu za mafuta kama alizeti na pamba, uzalishaji wa mazo ya kimkakati pamoja na huduma za ugani na kuahidi kuwa mambo hayo yamewekwa kwenye utekelezaji wa bajeti inayokuja ya mwaka 2021/2022.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa fedha na msisitizo umewekwa kwenye kuzalisha mazao ya mbegu za mafuta ili kupunguza utegemezi kwenye eneo hilo ambalo nchi imekuwa ikitumia zaidi ya shilingi bilioni 400 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.

Waziri Mkenda amesema kwa kuanzia Vituo vya Utafiti vitajikita katika kutafiti mbegu bora za mazao ya mbegu za mafuta ili kuja na mbegu bora lakini pia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kupitia mashamba yake; ASA itazalisha mbegu bora kwa wingi ambazo zitauzwa kwa Wakulima kwa bei nafuu.

Eneo lingine ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani kote nchini na kwa kuanzia Wizara imepanga  kuwawezesha Maafisa Ugani wa mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu kupata vitendea kazi kama kama pikipiki na kuwezeshwa pembejeo bora za kuanzisha mashamba darasa kwa kila Afisa Ugani.

“Pamoja na juhudi zote hizo lengo letu ni kuhakikisha tunatatua tatizo la masoko kwa Wakulima wetu lakini pia kuongeza uwekezaji kwa ujumla na ndiyo maana tunaona juhudi hizi tuwashirikishe na Sekta Binafsi ambayo itasaidia katika mageuzi katika kuendesha kilimo cha kisasa”. Amekaririwa Profesa Mkenda.

Kwa upande wake Balozi wa Uholanzi nchini Jeroen Verheul ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye Sekta ya Kilimo hususan kwenye uzalishaji wa mbegu bora za zao la viazi mviringo kupitia Mradi wa SHAWISHA unaotarajiwa kuanza baada ya kusimama kwa muda.

“Tutaendela kusaidia kwenye biashara ya mazao ya kilimo na uwekezaji kwa ujumla kwa sasa na kwa baadae hususan kwenye eneo la uzalishaji wa mbegu bora za viazi mviringo”. Amesisitiza Balozi Jeroen Verheul.

No comments:

Post a Comment

Pages