MAWAZIRI
wa Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana Jijini
Arusha katika mkutano wao wa 12 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa
Fedha na Uchumi ambapo, pamoja na mambo mengine wamekubaliana kutoivunja
Tume ya Kiswahili ya Jumuiya hiyo kutokana na umuhimu wa kukuza na
kutumia lugha hiyo kwa mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Uamuzi
huo umetokana na msimamo wa Tanzania na nchi za Kenya na Uganda ambazo
zimekataa mapendekeo ya mtaalamu mshauri aliyependekeza kuvunjwa kwa
tume hiyo na kupendekeza majukumu yake yasimamiwe na Idara ya Habari,
Teknolojia, Utamaduni na Michezo iliyopo Sekretarieti ya Jumuiya kwa
kushirikina na nchi wanachama ili kupunguza gharama za uendeshaji wa
Jumuiya hiyo.
Akichangia
hoja kuhusu kuvunjwa kwa Kamisheni ya Kiswahili yenye Makao yake Makuu
Zanzibar ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Jumuiya, Kiongozi wa
Ujumbe wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu
Nchemba (Mb) alisema kuwa hoja hiyo inalenga kudidimiza malengo na
misingi liyopo ya kuiunganisha jumuiya na kwamba ni wakati wa kuienzi
Kamisheni hiyo kwa kuifanyia mageuzi badala ya kufikiria kuivunja.
“Tusiongelee
suala la kiswahili kama lugha ya kufundishwa shuleni lakini tukione
Kiswahili kama lugha inayotuunganisha kama wanajumuiya ya Afrika
Mashariki” Alisisitiza Dk. Nchemba.
Aidha
katika kikao hicho, Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Fedha na Uchumi
wamekubaliana na mapendekezo ya mshauri elekezi kuhusu kupunguza idadi
ya wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka 9 kutoka kila nchi
wanachama hadi kufikia wabunge 5 ili kupunguza gharama za uendeshaji wa
Jumuiya pamoja na kuongeza ufanisi.
Katika Mkutano huo nchi wanachama ziliwasilisha miongozo na kauli mbiu za bajeti za nchi wanachama kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Mkutano
huo pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbambali
zilizowasilishwa kama vile taarifa za Kamati zinazoshughulikia masuala
ya Fedha ikiwemo ile ya Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Nchi
Wanachama pamoja na kufanya mashauriano ya awali ya Bajeti ya Mawaziri
wa Fedha na masuala ya Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kadhalika,
Mkutano huo umepokea Taarifa ya Utekelezezaji wa Maazimio mbalimbali
yaliyofikiwa wakati wa Mkutano wa 11 wa Baraza hilo la Kisekta pamoja na
taarifa ya Utafiti wa kuboresha Mifumo na Miundo ya Uendeshaji wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kulingana na rasilimali zilizopo.
Awali
akifungua mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Waziri wa Fedha wa Kenya,
Ukur Yatani Kanacho alitoa, pole kwa niaba ya Mawaziri walioshiriki
Mkutano huo kwa Ujumbe wa Tanzania na Serikali kwa ujumla kwa kuondokewa
na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli.
Aidha,
alitoa pole kwa Nchi Wanachama kufuatia janga la ugonjwa wa Corona
ambalo limeathiri uchumi wa Nchi nyingi na kuwataka wajumbe kuendelea
kushirikiana kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kadhalika
kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Dk. Nchemba alipokea salamu za pole
zilizotolewa na kusisitiza Nchi Wanachama kuendeleza umoja na mshikamano
kama njia mojawapo ya kumuenzi Hayati Dk. Magufuli.
Mkutano
wa Mawaziri umepitisha kwa kauli moja kauli mbiu ya mwaka wa fedha
2021/2022 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki isemayo “Economic Recovery
through Industralization and Inclusive Growth”.
Ujumbe
wa Tanzania kwenye Mkutano huo umewahusisha pia Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Uwekezaji Uchumi na Ajira Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga,
Waziri, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Jamal Kassim Ali,
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, Katibu Mkuu Ofisi
ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dk. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar, Mussa Haji Ali, Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamis Shaaban na Maafisa
Waandamizi kutoka Serikalini.
Mkutano
huo ambao umeitishwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
ulitanguliwa na kikao cha Ngazi ya Wataalam kutoka Sekta za Fedha na
Uchumi uliofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 Mei 2021 na kufuatiwa na
kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika Mei 6, mwaka huu.
Nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC zilizoshiriki mkutano huo ni
Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na nchi ya Sudani Kusini
haijahudhuria, ambapo nchi zilizoshiriki moja kwa moja kwenye mkutano
huo uliofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo Jijini Arusha ni Tanzania,
Uganda na Burundi wakati walioshiriki kwa njia ya mtandao ni Kenya na
Rwanda.
No comments:
Post a Comment