Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Ochola Wayoga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na Maadhimisho ya Juma la Elimu (Global Action Week for Education-GAWE) kwa mwaka 2021 yatakayofanyika Wilaya ya Rorya, mkoani Mara. Kushoto ni Afisa Uratibu wa TEN/MET, Alistidia Kamugisha akifuatilia. |
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) umetangaza kufanya maadhimisho ya Juma la Elimu (Global Action Week for Education-GAWE) kwa mwaka 2021 katika Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, huku ukiwataka wananchi na wadau wa elimu kujitokeza ili kuweza kushiriki kwenye maadhimisho hayo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na vyombo vya habari, Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga amesema shughuli za maadhimisho ya mwaka huu zitaanza rasmi Mai 31, 2021 hadi Juni 4, 2021 zikiambatana na mijadala ya wananchi kuhamasisha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto.
Bw. Wayoga alisema TEN/MET imeambua kupeleka maadhimisho ya Juma la Elimu wilayani Rorya kutokana na changamoto za elimu zinazojionesha kwa kiasi kikubwa eneo hilo, hasa kwenye matokeo ya mitihani kwa elimu ya msingi na sekondari kidato cha nne.
"...Wadau wa TEN/MET kwa kushirikiana na serikali na Halmashauri ya Rorya tunakwenda kuhamasisha wanafunzi, wazazi, waalimu na watumishi katika sekta ya Elimu kusimamia ufahulu na uwekezaji katika mifumo ya elimu kwa maendeleo endelevu. Ni matarajio yetu kuwa wana Rorya watakuwa tayari kuungana nasi katika jitihada hizi," alisema Wayoga.
Alisema lengo kuu la maadhimisho hayo mwaka huu ni kuhamasisha juu ya lengo endelevu namba 4 (SDG4) kwa ujumla wake kwa kuhakikisha elimu bora inatolewa kama sehemu ya haki, huku malengo mengine yakiwa ni kuongeza uelewa kwa umma juu ya madai ya haki ya elimu iliyo bora na kuhamasisha elimu kwa makundi maalumu kama vile watoto wenye ulemavu.
Aidha akitaja shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho hayo, alisema baada ya ufunguzi wa maadhimisho hayo Mai 31 kutakuwa na mikutano itakayofanyika vijiji mbalimbali na wananchi Juni Mosi na Pili kuwahamasisha wanajamii kushirikiana na Serikali katika kuboresha elimu iliyo jumuishi.
"Tarehe 3 Juni kutakuwa na Kongamano la Elimu kimkoa litakalofanyika wilayani Rorya na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu. Kwa wiki nzima kutakuwa na maonesho mbalimbali yakiendelea ndani ya uwanja wa Mji wa Shirati na Juni 4 itakuwa kilele cha maadhimisho hayo." Alisema Mratibu huyo wa TEN/MET Taifa.
Hata hivyo alisema lengo lingine la maadhimisho hayo itakuwa ni kuhamasisha jamii, Serikali na mashirika yasiyo na kiserikali umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika masuala ya elimu na utekelezaji wa lengo la maendeleo endelevu la nne na hasa kuimarisha mifumo ikiwemo ya kuwekeza katika TEHAMA.
No comments:
Post a Comment