HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 18, 2021

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFUNGUA KIWANDA CHA USHONAJI CHA JESHI LA POLISI TANZANIA -KURASINI

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akivuta utepe kufungua Kiwanda cha Ushonaji cha Jeshi la Polisi Tanzania kilichopo Kurasini mkoani Dar es Salaam leo tarehe 18 Mei, 2021. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Khamis Hamza Khamis pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro. 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipiga makofi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Khamis Hamza Khamis pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro mara baada ya kukata utepe kuashiria ufunguzi wa Kiwanda cha Ushonaji cha Jeshi la Polisi Tanzania kilichopo Kurasini mkoani Dar es Salaam leo tarehe 18 Mei, 2021.

  

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akikagua kazi mbalimbali zinazofanywa katika kiwanda hicho cha ushonaji cha Jeshi la Polisi Tanzania kilichopo Kurasini mkoani Dar es Salaam mara baada ya kukifungua leo tarehe 18 Mei, 2021. 

  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akikagua kazi za upimaji na ukataji wa vitambaa vinavyotumika katika kushona sare za Jeshi la Polisi katika Kiwanda cha Ushonaji Nguo cha Jeshi la Polisi Tanzania kilichopo Kurasini mkoani Dar es Salaam.

  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa na Jeshi la Polisi Kurasini mkoani Dar es Salaam mara baada ya kufungua Kiwanda hicho cha Ushonaji.

  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Askari pamoja na Maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi pamoja na Wageni wengine Kurasini mkoani Dar es Salaam mara baada ya kufungua Kiwanda cha Ushonaji cha Jeshi la Polisi Tanzania. PICHA NA IKULU.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 18 Mei, 2021 amefungua kiwanda cha ushonaji bohari kuu ya Jeshi la Polisi kilichopo Kurasini Mkoani Dar es Salaam.

Kiwanda hicho kimejengwa kwa utaratibu wa nguvu kazi (force account) kwa gharama ya shilingi Milioni 666.4 badala ya shilingi Bilioni 1.4 kama kingejengwa kwa utaratibu wa zabuni.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IJP Simon Sirro amesema ujenzi wa kiwanda hicho umepanua uwezo wa kiwanda kutoka vyerehani 70 hadi 130 vyenye uwezo wa kushona sare 125,000 za Askari kwa mwaka.

IJP Sirro amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kufungua kiwanda hicho na amesema Jeshi la Polisi linapanga kuanzisha shirika la uzalishaji litakaloendesha miradi mbalimbali kikiwemo kiwanda cha ushonaji, kiwanda cha kuzalisha maji na usindikizaji wa fedha.

Pia, IJP Sirro amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa Serikali kutoa shilingi Bilioni 6 kwa ajili ya kuwalipa wastaafu wa Jeshi la Polisi ambao wameanza kulipwa.

Akizungumza na Maafisa wa Polisi, Askari na viongozi mbalimbali katika uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Mhe. Rais Samia amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kujenga kiwanda hicho kwa kutumia mapato yake ya ndani na kwa kutumia nguvukazi iliyotumia kiasi kidogo cha fedha ikilinganishwa na endapo lingetumia wazabuni.

Mhe. Rais Samia ameelezea kufarijika kwake kukifungua kiwanda hicho ambacho kiliwekwa jiwe la Msingi na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na amesema kukamilika kwa kiwanda hicho ni uthibitisho wa kumuenzi Hayati Dkt. Magufuli.

Ameelekeza Majeshi mengine kushona sare zao katika kiwanda hicho na pia kujielekeza kushona sare nyingine kama vile viatu badala ya kila Jeshi kushona aina ileile ya sare zinazoshonwa na Jeshi lingine ili kudhibiti uagizaji wa sare za Askari kutoka nje ya nchi.

Aidha, Mhe. Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kujielekeza kudhibiti matukio ya uhalifu na uvunjaji wa sheria ikiwemo makosa ya usalama barabarani badala ya kujikita katika kutoa adhabu ama kuwa kitega uchumi.

Amelitaka jeshi hilo kuongeza juhudi katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu ambavyo vimeanza kujitokeza na ameonya kuwa katika upandishaji wa vyeo, uteuzi na kutengua uteuzi wa Maafisa wakiwemo Makamanda wa Polisi wa Mikoa kipimo cha juhudi za udhibiti wa matukio ya uhalifu hasa ujambazi kitatumika.

Mhe. Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuweka mfumo utakaowezesha kutambuliwa kwa wavunja sheria za usalama barabarani popote walipo hapa nchini ili ikitokea dereva kafanya makosa katika mkoa mmoja aonekane katika mkoa mwingine na achukuliwe adhabu stahiki ikiwemo kufutiwa leseni.

Amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kupunguza msongamano wa Mahabusu waliokamatwa kutokana na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaachia wenye kesi za kubambikizwa kama ambavyo imefanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambayo imefuta kesi 147 za rushwa za kubambikizwa.

Mhe. Rais Samia ameagiza sheria inayolazimu majeruhi kuwa na fomu ya PF3 ndipo wapatiwe matibabu katika vituo vya tiba irekebishwe ili majeruhi wasikoseshwe matibabu pale wanapokuwa hawana fomu hiyo.

Mhe. Rais Samia ameahidi kufanyia kazi changamoto mbalimbali za Jeshi la Polisi kadiri Serikali itakavyokuwa na uwezo wa kifedha.

No comments:

Post a Comment

Pages