Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam , Amos Makalla ameanza rasrmi majukumu yake kwa kukutana na Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi wa mkoa huo na kuahidi kushirikaina nao bega kwa bega ili kuendelea kuchochea maendeleo.
Aidha, amesema ataweka utaratibu wa kukutana na wazee wa chama hicho kila baada ya miezi mitatu kujadili masuala mbalimbali yawahusuyo na kupokea ushauri kutoka kwa wazee hao.
Amesema ameamaua kukutana nao kwani anatambua thamani na Mchango wa Wazee Katika jamii hivyo ameona ni vyema kuanza majukumu yake kwa kukutana nao ili kuchota busara na Baraka zao kwani anatambua Wazee ni hazina muhimu.
Amebainisha kuwa kutatua kero na changamoto za Wananchi atawaeka utaratibu kukutana na wanananchi wa kata zote za Dar es Salaam ili kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzipatia majibu.
Amesisitiza kuwa mkoa huo ni mkubwa na wenye taswira ya nchi nzima katika nyanja mbalimbali, hivyo amejipanga kuhakikisha Jiji linakuwa shwari na watu wanafanya shughuli zao pasipo usumbufu wowote Kama maono na mategemeo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza Wazee wa chama hicho, Hemed Mkali amesema wanaahidi kumpatia ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake na kumpongeza RC kwa namna anavyowaheshimu na kuwathamini.
Naye Mjumbe wa baraza la wazee hao kutoka Wilaya ya Kinondoni Janeth Kahama amesema wanamtakia kila la kheri katika shughuli zake na kwamba wataendelea kumuunga mkono ili afikikie malengo aliyojiwekea katika mkoa huo.
Balozi Mstaafu Chrispoher Liundi amesema watajitahidi kufanya kazi na RC huyo bega kwa bega na kumuomba kuweka mahusiano mazuri na kundi hilo na kuwasisitiza wazee hao endap0 kuna dosari wasisite kueleza ila kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Ramadhan Madabida amesema wapo tayari kumuunga mkono na kwamba wanafahamu uwezo wa RC Makalla tangu alipoanza kuitumikia CCM hivyo amemuomba afikishe salamu kwa Rais Samia ya kuunga mkono jitihada zake za kiuongozi.
No comments:
Post a Comment