HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 26, 2021

RC MAKALLA AONYA MAJAMBAZI DAR AAGIZA POLISI KUYAKAMATA


 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa huo, Amos Makalla, akizungumza kuhusiana na watu wanaojihusisha na ujambazi na kuliagiza Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam kuwashughulikia kikamilifu majambazi na vibaka jijini humo.  

 

Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa huo , Amos Makalla amewaonya watu wanaojihusisha na ujambazi na kuliagiza Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwashughulikia kikamilifu majambazi na vibaka jijini humo. 

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kutokea matukio ya ujambazi katika eneo la Mbezi ambapo majambazi walisababisha kifo cha mtu mmoja aliyekuwa akitoka benki kuchukua fedha na kwamba tukio la pili lilitokea Mabibo na kwamba majambazi walimjeruhi mfanyabiashara katika harakati za kutaka kumpora fedha zake.

Aidha, amewataka watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha polisi mara moja na kwamba watakaokaidi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

RC  huyo ameliagiza jeshi hilo kuanza kwa operesheni ya kufagia watu wote wanaofanya uhalifu mkoani humo ambapo amewaomba wazazi kufuatilia mienendo ya watoto kwa kuwakanya endapo wanashiriki waache kushiriki.

Amesema kwakuwa uzoefu unaonyesha wahalifu  hutumia silaha kujeruhi na kusababisha vifo,  hivyo  ni vyema jeshi hilo likawachukulia hatua kikamilifu kabla hawajazitumia katika uporaji na mauaji wakati wakiwa kwenye matukio ya ujambazi.

Amewahikikishia wananchi usalama na kuwataka kuendelea kufanya shughuli zao kama kawaida kwani vyombo vya ulinzi na usalama viko macho kuwashughulikia wale wote wenye nia ya kuhatarisha usalama wa wakazi na mali zao.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam Camilius Wambura amesema Katika msako ulioanza Mei 21 hadi Mei 25 wamefanikiwa kuwakamata Majambazi na vitu mbalimbali ikiwemo magari manne, pikipiki moja, bunduki moja, laptop na vifaa vinginevyo.

Aidha Kamanda Wambura amesema kuwa maagizo yaliyotolewa wameyapokea kwa mikono miwili na watayafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa.


Kamanda huyo amewaonya wahalifu wanaoshindana na vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kujidanganya kwani mkono wa sheria ni mrefu.

No comments:

Post a Comment

Pages