HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 28, 2021

Marie Stopes, Lavy Pads washerehekea hedhi salama

 

Baadhi ya wafanyakazi wa Marie Stopes na Lavy Pads wakigawa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Kiembesamaki Mjini Zanzibar wakati wa kuadhimisha siku ya hedhi salama visiwani humo leo Mei 28. 2021.



Na Irene Mark


Siku ya hedhi duniani huadhimishwa kila mwaka, siku ya tarehe 28 Mei. Siku hii ina lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa dhumuni la kuongeza uelewa kuhusu maswala ya hedhi  na kuhamasisha upatikanaji maji safi na taulo (visodo)  kwa wasichana/wanawake hasa wale walio katika mazingira  magumu  ili wanapoingia katika siku zao za hedhi  waweze kujisitiri na kuendelea na shuguli zao kama kuhudhuria masomo na shughui nyingine.
 
Hedhi ni nini ?
Ni kipindi maalumu katika mzunguko wa mwanamke mwenye umri wa kuzaa. Wakati huo, ambao kwa kawaida unarudi kila baada ya mwezi mmoja hivi, yeye hutokwa na damu kwenye uke. Sababu ya damu kutoka ni kwamba, kijiyai kilichokomaa na kutoka nje ya kifuko cha vijiyai kisipopata mbegu ya mwanamume baada ya siku moja kinaharibika harakaharaka; hapo ngozi nyembamba ya tumbo la uzazi, iliyotanuka kwa damu ili kupokea na kulisha mimba, inajiengua  na kutoa damu.
Kumbe mbegu ikikifikia kijiyai, mimba inapatikana na kujishikiza kwenye kuta za tumbo la uzazi ili iendelee kukua; hapo damu haitoki na mama anaweza kujihisi mja mzito.Mizunguko mingi ya hedhi huwa na siku kadhaa za mwanzo ambapo mimba haiwezi kupatikana (muda wa kutoshika mimba kabla ya kudondosha kijiyai), halafu siku ambazo mimba inaweza kutungika, na kisha siku kadhaa tu kabla ya hedhi ambazo mimba haiwezi kutungika (muda wa kutoshika mimba baada ya kijiyai kudondoshwa).
Hedhi salama nini ?


Hedhi salama ni ile ambayo inahusisha mtoto wa kike/mwanamke kupata mahitaji yake yote muhimu akiwa kwenye siku zake za hedhi. Mahitaji hayo huhusisha taulo za kike ama pedi kama ijulikanavyo na wengi, maji safi na salama na sehemu ya kubadilishia. Wataalamu wa afya wanasema kuwa mtoto wa kike akipata hedhi salama basi ataweza kuondokana na matatizo mengi ya kiafya kama vile miwasho, fangasi pamoja na magonjwa mengine na hivyo huwa hedhi yenye amani na furaha.


Suala la hedhi halipaswi kuwa kero kwa mtoto wa kike. Hata hivyo, imekuwa tofauti kwa watoto wengi wa kike ambao wamekuwa wakipata wasiwasi na kukosa raha pindi wanapokaribia mzunguko wao. Hii inatokana na changamoto ambazo watoto hawa wa kike wanazopitia katika kupata hedhi salama.
Jambo la kusikitisha ni kwamba mara nyingi tumekuwa tukigusia tu masuala ya kiafya pindi tunapozungumzia hedhi salama na kusahau kuwa kukosekana kwa jambo hili kunaweza kuleta athari katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanamke huyu.  Baadhi ya mazingira yanayoweza kumkwamisha mtoto wa kike ni pamoja na:

Kutojihusisha katika shughuli mbalimbali za jamii kutokana na kukosekana kwa nyenzo ambazo zitamsaidia mtoto wa kike katika kipindi aonapo hedhi basi mara nyingi watoto hawa hujitenga katika shughuli mbalimbali kama vile shule, kazi, michezo, mikutano mbalimbali kwani huona aibu na hofu ya kuonekana kwa watu akiwa  na hali ile. Kutojihusisha na shughuli hizi huweza kuleta madhara makubwa sana kwa mtoto huyu wa kike na yanaweza kuwa ya papo kwa papo au ya muda mrefu.

Kukosa fursa kama mwanamke atakuwa wa kukaa tu nyumbani kipindi akiwa kwenye siku zake sababu tu amekosa vitu vya kumsaidia kupata hedhi salama basi ni wazi kuwa atakuwa anakosa fursa nyingi sana zinazoweza kujitokeza katika jamii yake kipindi yeye akiwa katika siku zake za hedhi
 
 
Ni kwa jinsi gani hedhi salama inahusiana na haki za binadamu?

Ni wazi kuwa kila mtu ana stahili haki za kimsingi bila kuangalia cheo wala taifa wala tabaka, wala jinsia, wala dini; anapaswa kufaidi haki zake za msingi kwa sababu tu yeye amezaliwa binadamu. Kuna baadhi ya haki za binadamu ambazo  mtoto wa kike atazikosa ikiwa tu hedhi salama itakosekana.

Haki kuthaminiwa utu wake, ikiwa mwanamke atakosa nyenzo ambazo zinzaweza kumsaidia kupata hedhi salama basi ni wazi utu wake kwa watu wengine wanaomtazama utashuka hasa kwa wale wasiolewa suala lake pindi watapomtazama. Embu fikiria maoni ya watu katika jamii yako yatakavyokuwa pindi watakapomuona msichana akitembea nguo yake ikiwa imechafuka na damu ya hedhi. Ni wazi katika jamii yetu ya hapa Tanzania wengi watamtazama kwa kumdharau na kumkebehi na ile aibu atakayoipata basi itaponza utu wake.

Haki ya kuwa kupata matibabu stahiki na kuwa na afya bora, wanawake wanaweza kukumbwa na matatizo mbalimbali ya kiafya pindi watakoshindwa kupata nyenzo muhimu za kuwasaidia wakati wakiwa katika siku zao za hedhi. Wanaweza pata fangasi, miwasho, maumivu sehemu zao za siri pamoja na madhara ya kisaikolojia yanayotokana na hali ya unyonge na aibu ya kujua madhara hayo yametokana na wao kukosa vifaa muhimu vya kujisitiri vinaweza kumfanya aone aibu kwenda kwenye kituo cha afya ili kupata matibabu.

Haki ya kupata elimu, mtoto wa kike anaweza shindwa kupata haki yake ya kupata elimu pindi awapo katika siku zake za hedhi kwa kuwa tu amekosa vitu vya kumsitiri kipindi hicho. Kipindi hicho kwake huwa kigumu kwani hushindwa kuhudhuria shule hali inayoweza pelekea matokeo mabaya na muda mwingine hata adhabu kwa walimu wasioelewa mazingira anayopitia binti huyu.

Haki ya kufanya kazi, kukosekana kwa vitu muhimu vya kujisitiri kwa mtoto wa kike kunaweza mpelekea akashindwa kufanya kazi au kupoteza fursa mbalimbali za kazi. Mwanamke huyu atalazimika kubaki nyumbani kwa muda wote atakaokuwa katika siku zake za hedhi na matokeo yake yanaweza kuwa ni kupoteza nafasi ya kazi au malipo aliyopaswa kupata kutokana na kazi hiyo. Embu fikiria wale watu wanaofanya kazi za malipo ya kila siku, ni wazi kuwa suala hili litaathiri kazi na kisha kipato chake.

Haki ya kutokubaguliwa na mtu au chombo chochote katika kutekeleza majukumu yake, Mwanamke anaweza kubaguliwa na watu wanaomzunguka pindi atakapokosa nyenzo muhimu za kujistiri akiwa katika siku zake. Jaribu kufikiria wale watu ambao bado wana imani potofu kuhusu damu ya hedhi ya mwanamke kuwa ni sumu na inaweza kusababisha mimea kukauka, chakula kuchacha, pombe kuwa chungu nk, anaposhuhudia damu ya hedhi ya mwanamke imesambaa kwenye nguo zake, ni wazi kuwa atamtenga na kumbagua. Na ubaguzi huo unaweza jitokeza katika mashule, na hata shughuli mbalimbali za jamii.

 
Kwanini wavulana kushiriki kwenye masuala ya hedhi ?
Ni muhimu wavulana kushiriki kupata Elimu ya musuala ya hedhi  kama washiriki wenza na kiini cha mabadiliko .
 
Maadhimisho ya siku ya hedhi


Katika kuadhimisha siku ya hedhi duniani , shirika la Marie stoipes Tanzania kushirikiana na Lavy Limited Company watatembelea baadhi ya shule na kutoa Elimu ya masuala ya hedhi kwa wasichana lakini  ushirika huu utaweza kuwashika mkono wasichana kwa kutoa  Zawadi mbalimbali ikiwemo taulo za kike.
 
Wito
Kwa mashirika ya afya ,  mashirika ya maendeleo na taasisi mbalimbali kuzisaidia jamii kwa namna mbalimbali  kuhakikisha wasichana hasa walio mashuleni wanakuwa na mazingira rafiki ili wanapoingia kwenye siku zao za hedhi wasikose mahitaji yao muhimu yatakayowasababisha kushindwa kushiriki kwenye masomo na masuala mengine ya jamii kutokana na hedhi.


Kuliangalia suala la upunguzaji wa garama za taulo za kike, upatikanaji wa maji safi na salama katika shule , kusaidia maeneo yenye uhitaji ili wasichana waweze kupata taulo za kujisitiri kwa muda wa mwaka mzima ili wasiweze kukosa mahudhurio shuleni.
 
Ushauri
Kwa wasichana wanaokutana na changamoto za hedhi ikiwemo maumivu yasiyo ya kawaida basi watembelee vituo vya afya vilivyo karibu nao kwa msaada zaidi. Lakini pia wanaweza kutupigia Marie stopes bure 0800 753 333 kwa ajili ya ushauri wa masuala ya hedhi na wanaweza pia kutembelea vituo vyetu vilivyopo Dar es salaam, Zanzibar, Mwanza, Musoma, Kahama, Arusha , Iringa , Mbeya na Kimara .

No comments:

Post a Comment

Pages