HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 11, 2021

SERIKALI YAJA NA ELIMU MBADALA KWA WANAFUNZI WANAOPATA MIMBA SHULENI

 Waziri wa Serikali ya Uingereza anayeshugulika na mambo ya Afrika, James Duddridge (katikati), akipata maelezo wakati alipofanya ziara katika Shule ya Sekondari Kibasila jijini Dar es Salaam leo Mei 11, 2021. Kulia ni Balozi wa Uingereza nchini, David Concar na wapili kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.



Waziri wa Serikali ya Uingereza anayeshugulika na mambo ya Afrika, James Duddridge akizungumza na wanafunzi wa kidato cha tano Shule ya Sekondari Kibasila jijini Dar es Salaam leo Mei 11, 2021.


Waziri wa Serikali ya Uingereza anayeshugulika na mambo ya Afrika, James Duddridge, akipata maelezo kutoka kwa mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Kibasila, Asha Shabani, alipotembelea maabara ya shule hiyo jijini Dar es Salaam leo Mei 11, 2021. Katikati ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.


Balozi wa Uingereza nchini, David Concar (kushoto), akifafanua jambo wakati wa ziara ya kutembelea Shule ya Sekondari Kibasila Dar es Salaam.

 

Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuja na mpango wa Elimu mbadala kwa wanafunzi wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni kupata fursa ya kurudi na kuendelea na Masomo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ziara ya Waziri wa Serikali ya Uingereza anayeshugulika na Mambo ya Afrika James Duddridge, katika Shule ya Sekondari Kibasila jijini Dar es Salaam.

Waziri Ndalichako alisema Serikali imejipanga kuhakikisha wanafunzi wanaokatisha masomo yao kwa kupata mimba wakati wa masomo kurejea na kuendelea na masomo kwa mfumo wa Elimu mbadala.

"Tumeweka utaratibu kwa watoto ambao wanapata ujauzito kuendelea na masomo yao kupitia njia ya Elimu mbadala ambapo katika mfumo huo, inategemea ameacha Shule akiwa kidato gani ama darasa gani kwa mfano ameacha akiwa kidato cha kwanza anaweza akasomo kupitia mfumo wa Elimu mbadala akifika kidato cha pili  akafanya mtihani akafaulu anaweza kurudi katika mfumo wa kawaida.

"Vilevila yule ambae labda anakuwa ameacha akiwa kidato cha tatu akifanya mtihani wake kupitia mfumo usio rasmi akafaulu mtihani wa kidato cha nne anapata nafasi fursa sawa kama yule ambaye amekuwa shuleni kupangiwa shule yoyote kulingana na ufaulu wake." Alisema Waziri na kuongeza kuwa.

"Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha tunasimamia Elimu kwa watoto wa kike na kuondoa vikwanzo ambavyo vinasababisha watoto wa kike wasifanye vizuri katika masomo yao sambamba na kuboresha Elimu kwa ujumla kwa watoto wa kike na wakiume ili wapate Elimu bora.

Akizungumzia ziara ya Waziri wa Serikali ya Uingereza anayeshugulika na Mambo ya Afrika Prof. Ndalichako alisema Waziri huyo amekuja nchini kuangalia mambo mbalimbali huku akibainisha kuwa amemleta mwaliko wa kuhudhuria mkutano unaohusiana na Ushirikiano katika Elimu.

"Katika mkutano huo mambo yatakayo zungumziwa ni pamoja na namna ambavyo nchi zinahakikisha zinatekeleza jukumu lake la msingi la kutoa elimu iliyo bora kwa wananchi wake lakini pia na kuangalia zaidi elimu kwa mtoto wa kike.

"Na amekuwa anapenda kufahamu jinsi ambavyo kama nchi timepiga hatua au ni hatua gani ambazo tunachukua kuhakikisha kwamba mtoto wa kike anapata elimu iliyo bora. Kwa hiyo niseme kwanza Uingereza ni nchi ambayo tumekuwa tunashirikiana nayo vizuri kwenye sekta ya Elimu.

Kwa upande wa Waziri wa Serikali ya Uingereza anayeshugulika na Mambo ya Afrika James Duddridge aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya Elimu kwa watoto wa kike.

"Niko hapa kuangalia malemgo na mikakati ya Elimu jinsi gani inaboreka ama tunaiboreha na kufikia viwango vya juu, tukiwa tunatambua hapa Tanzania kuna mfumo wa Elimu bure.

"Asubuhi ya leo (jana) nimeonana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na kujadili jinsi gani mpango wa Elimu unaenda kuboreka pamoja na kuajiri walimu wapya, lakini pia nimemualika Waziri wa Elimu katika Mkutano ambao utajadili masuala mbalimbali katika mashirikiano kwenye sekta ya Elimu ili kusaidia kuondoa changamoto zinazoikumba sekta ya hiyo."alisema Duddridge.


Waziri huyo anaendelea na ziara yake ya siku mbili ambapo ataimalizia Zanzibar ambako atakutana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi kuzungumzia masuala mabalimbali ya kimaendeleo na mashirikiano.

No comments:

Post a Comment

Pages