Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Redemptha Matindi akizungumza na wauguzi wakati wa ufunguzi wa kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya waaguzi duniani ambayo kitaifa inatarajiwa kufanyika mkoani Manyara Mei 12 mwaka huu.
NA ASHA MWAKYONDE, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Wauguzi Tanzania (TANNA), kimesema kuwa idadi ya wauguzi na wakunga bado haijafikia kiwango kinachostahili kutoa huduma stahiki na ni changamoto inayokikabili chama hicho.
Hayo yalisema jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Redemptha Matindi wakati wa ufunguzi wa kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya waaguzi duniani ambayo kitaifa inatarajiwa kufanyika mkoani Manyara Mei 12 mwaka huu.
Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Alisema kuwa kuna idadi kubwa ya wastaafu ambao ni wauguzi na wakunga hali inayofanya idadi hiyo kuzidi kupungua na kwamba ni changamoto kwa watoa huduma hao.
Matindi alisema kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha kuanzia pale mkunga anayetengenezwa bado haijawa nzuri vyuoni na kuweza kufikia kiwango.
"Pia idadi kubwa ya wagonjwa wanaokwenda hospitali kwa wakati mmoja ikilinganishwa na idadi ndogo ya watoa huduma ya uuguzi na wakunga " alisema Matinda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TANNA tawi la Mloganzila Wilson Fungameza ambaye ni muuguzi alisema wameungana na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-(MHN), ili kuweza kujadili changamoto zao kwa pamoja.
"Tupo hapa kwa ajili ya kuazimisha siku hii muhimu ya wauguzi duniani sisi tumewahi lengo ni kujadili changamoto zetu na kuwasilisha matukio mbalimbali kabla ya Mei 12 ambapo kilele chake, "alisema.
Aliongeza kuwa mada zilizowasilishwa zitasaidia katika kukuza taaluma uuguzi na kwamba itasaidia kuboresha afya za wagonjwa.
No comments:
Post a Comment