HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 06, 2021

Mkataba wa huduma kwa mteja wazinduliwa Dodoma

Naibu Waziri Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa mteja uliofanyika jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojiahiyo Dkt. Leonard Akwilapo, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa mteja uliofanyika jijini Dodoma.

HAMIDA RAMADHANI, DODOMA



NAIBU Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga amezindua Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao una lengo la kuboresha utendaji kazi kwa watumishi wa Wizara hiyo .

Pia amesema mkataba huo wa huduma kwa mteja utalenga hasa katika kutoa huduma kwa wateja ambao ndio wadau wakubwa wa wizara hiyo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa  Mkataba huo leo Jijini hapa Naibu Waziri  huyo  amewaonya watumishi  wa Wizara ya hiyo watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao  kwa kufuata mkataba wa huduma kwa mteja unavyoelekeza  watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

"Niseme wazi kwa wale ambao watafanya vizuri katika kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia mkataba huo watatambuliwa kwa kupewa tuzo na wale wasiozingatia mkataba huo pia hatutasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu," amesema Kipanga.

Aidha amesema Mkataba huo unalenga kupunguza kama siyo kumaliza kabisa changamoto zinazoikabili wizara hiyo.

" Hivyo basi watumishi wa Wizara ya Elimu mnapaswa kuutekeleza mkataba huu wa huduma kwa mteja kwa weledi mkubwa katika kuhakikisha huduma katika Wizara ya Elimu zinaendelea kuboreka  ili kuiwezesha wizara yetu kujua namna ya kutatua changamoto zao," amesema Kipanga.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo amesema, utekelezaji wa mkataba huo ufungue  ukurasa mpya wa uwajibikaji kwa watumishi wa wizara hiyo katika kuwahudumia wananchi.

"Mkataba huo umeainisha aina za huduma zinazotolewa na wizara, wateja wanao wahudumia na viwango vya ubora kwa lengo la kuimarisha na kuboresha mahusiano yao na wateja," amesema Dkt Akwilapo.

Awali Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Moshi Kabengwe amesema mkataba huo ni chombo kinachowezesha mawasiliano mazuri kati ya mtoa huduma na anayepokea huduma.

Pia amesema pamoja na mambo mengine mkataba huo unaeleza ubora na viwango vya huduma zinazotolewa na unatoa mrejesho kutoka kwa wateja ili wizara iweze kufahamu huduma zinazotolewa kwa wateja.

No comments:

Post a Comment

Pages