Na Lydia Lugakila, Bukoba
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amekabidhi rasmi ofisi za mkoa tayari kuelekea Mtwara kituo chake kipya cha kazi, Brigedia Gaguti amekabidhi ofisi hiyo kwa Meja Jenerali Charles Mbuge.
Hafla ya makabidhiano rasmi ya ofisi kati ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti na Meja Jenerali Charles Mbuge yamefanyika katika ukumbi wa mkoa huo na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo zikiwemo taasisi za dini.
Akikabidhi rasmi nyaraka za kiofisi Brigedia Jenerali Gaguti amewashukuru wananchi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo kwa ushirikiano katika shughuli za maendeleo zilizopelekea mkoa huo unakuwa wa kiwango cha tofauti.
"Nimefanya kazi Kagera miaka 2 nawashukuru wana Kagera wapatao takribani milioni 3.1 kwa kipindi ambacho nimekuwepo Kagera nimeshiriki mambo mengi na makubwa ya kimaendeleo, wapo wengi walionisaidia katika majukumu yangu nimeuacha mkoa salama muendelee kuniombea ninapoelekea mkoani Mtwara kituo changu kipya cha kazi wana Kagera niwaombe mkampatie ushirikiano wa kutosha kwa asilimia 200 Ila nitabaki kuwa mwana Kagera licha ya kuwa mwana Mtwara" alisema Brigedia Gaguti.
Gaguti ameongeza kuwa hakujutia kuwepo katika mkoa huo kwani amejifunza mambo mengi ikiwemo kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi na kumuomba mkuu mpya wa mkoa huo meja jenerali Charles Mbuge kumalizia changamoto kubwa kwa wananchi hao ikiwemo ujenzi wa soko, stendi ya magari ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam tawi la Kagera na kuahidi ushirikiano kwa Meja Jenerali Mbuge.
Aidha baada ya makabidhiano hayo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge ameahidi ushirikiano kwa viongozi mbalimbali wa mkoa huo ikiwemo kusimamia haki, kusimamia maendeleo katika ukusanyaji wa mapato kwa halmashauri zote, huku akiwataka watendaji wake kutoa huduma nzuri kwa kutambua kuwa ofisi za serikali si za nyumbani kwao kwamba zifungwe watu wasiingie.
" Ili kiongozi ufanye kazi vizuri unatakiwa kuondoa ubinafsi mimi huwa najishusha nikiwa kazini ili mambo yasonge mbele kumbukeni taifa letu hatuna mjomba wala wala babu ni sisi wenyewe kikubwa tuwe wawazi na maendeleo yanaletwa na sisi hivyo hatuhitaji kusukumwa" alisema meja jenerali Charles Mbuge.
Jenerali Mbuge ameahidi kushirikiana na uongozi wa CCM ili kuendelea kutekeleza ilani ya chama ambayo inalenga kuwaletea maendeleo wananchi wa mkoa huo.
Hata hivyo kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawilo amempongeza mkuu wa mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti kwa uongozi wake mzuri kwa wanakagera na kuwataka watumishi wa mkoa huo kuendelea kuwatumikia wananchi ili wilaya hizo ziweze kuwa na maendeleo huku akimkaribisha mkuu mpya wa mkoa huo.
Naye mwakilishi wa wazee mkoani humo Suleiman Kabyemela mwenye umri wa miaka 94 amesema " Brigedia Gaguti sisi wazee wa Kagera na wanakagera kwa ujumla ingewezekana tungesema subiri tunashukuru kwa yote uliyotutendea kwa wakati wote uliokuwa hapa unakokwenda tunamuachia mwenyezi Mungu, Mbuge tunakukaribusha sana waswahili husema karibu mgeni mwenyeji apone"alisema mzee Kabyemela.
Ikumbukwe kuwa mnamo Mei 15 mwaka huu Rais Samia Suruhu Hassan alifanya mabadiliko na uteuzi kwa baadhi ya wakuu wa mikoa hapa nchini ambapo aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti alihamishiwa mkoani Mtwara na Kagera kukabidhiwa kwa Meja Jenerali Charles Mbuge.
No comments:
Post a Comment