Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo mkoani Kigoma wakati alipofika mkoani hapo akielekea wilayani Kasulu kuzungumza na wafanyabiashara kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zilizojitokeza hivi karibuni.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye wakati alipofika mkoani hapo akielekea wilayani Kasulu kuzungumza na wafanyabiashara kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zilizojitokeza hivi karibuni.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata akizungumza na viongozi wa wafanyabiashara wa wilayani Kasulu na Kigoma wakati wa mkutano wa viongozi hao uliofanyika Wilaya ya Kasulu kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zilizojitokeza wilayani humo hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Kigoma Bw. Raymond Ndabhiyegetse akizungumza wakati wa mkutano wa viongozi wa wafanyabiashara wa Wilaya ya Kasulu na Kigoma na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Aliphayo Kidata uliofanyika wilayani Kasulu kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zilizojitokeza wilayani humo hivi karibuni.
Katibu wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wa Wilaya ya Kasulu akizungumza wakati wa mkutano wa viongozi wa wafanyabiashara wa Wilaya ya Kasulu na Kigoma na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata uliofanyika wilayani Kasulu kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zilizojitokeza wilayani humo hivi karibuni.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo mkoani Kigoma wakati alipofika mkoani hapo akielekea wilayani Kasulu kuzungumza na wafanyabiashara kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zilizojitokeza hivi karibuni.
Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kigoma wakiwa kwenye kikao na Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Alphayo Kidata wakati alipopita mkoani hapo akielekea wilayani Kasulu kuzungumza na wafanyabiashara kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zilizojitokeza hivi karibuni. (PICHA ZOTE NA TRA).
*************************************
NA MWANDISHI WETU, KASULU
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata amezungumza na viongozi wa wafanyabiashara wa wilayani Kasulu na Kigoma ambapo ameambatana na baadhi ya viongozi waandamizi kutoka TRA Makao Makuu akiwemo Kamishna wa Kodi za Ndani Bw. Hebert Kabyemela, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo na Naibu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa Bw. Beatus Nchota.
Pamoja na viongozi hao waandamizi, Kamishna Mkuu Bw. Kidata amekwenda na timu ya watalaam wa kutoa elimu na huduma kwa mlipakodi kwa lengo la kutatua changamoto zilizojitokeza wilayani humo na kuhakikisha wanapita kila duka yaani mlango kwa mlango kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu sheria na taratibu za ulipaji kodi.
Kamishna Mkuu Kidata aliwaambia viongozi hao kwamba, ni muhimu kila upande yaani wafanyabiashara na watumishi wa TRA kuzingatia haki na wajibu wao kila wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Sisi watumishi wa TRA tunafanya kazi kwa kufuata misingi yetu ya maadili ambayo ni uwajibikaji, uadilifu na weledi lakini pia kama mmoja wenu alivyosema, ni lazima pia sote, ninyi na sisi TRA tuzingatie haki na wajibu kila tunapotekeleza majukumu yetu,” alisema.
Kwa upande wa viongozi hao, walisema wamefurahishwa na kitendo cha Kamishna Mkuu wa TRA kufika wilayani hapo na kufanya nao mazungumzo pamoja na kupeleka timu ya watalaam kutoa elimu kwa walipakodi hao kwa lengo la kutatua changamoto zilizojitokeza baina ya wafanyabiashara wa wilayani Kasulu na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
“Ndugu Kamishna Mkuu, tunakushukuru sana kwa kuja kuzungumza na sisi na tumefurahi sana kwa kutuletea watalaam wa kutuelimisha na kutatua changamoto za mfanyabiashara mmoja mmoja kama zilivyowasilishwa kwako leo,” alisema Bw. Prosper Guga ambaye ni Katibu wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wilayani Kasulu.
Kabla ya kuzungumza na viongozi hao wa wafanyabiashara wa Kasulu, Kamishna Mkuu Bw. Alphayo Kidata alipata nafasi ya kuwatembelea baadhi ya viongozi wa serikali mkoani Kigoma ambapo alifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Samson Anga na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe. Kanali Simon Anange.
Aidha, Kamishna Mkuu huyo alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa TRA wa Mkoa wa Kigoma na kuwataka kuzingatia kufanya kazi kwa bidii na weledi ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati na hiari huku wakiwapatia elimu ya kodi.
Hivi karibuni, wafanyabiashara wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma walifanya mgomo wa kufunga maduka wakidai kuwa watumishi wa TRA wilayani humo hawana lugha nzuri na wanawakadiria makadirio makubwa suala linalowapelekea kushindwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, kutokana na mazungumzo yaliyofanyika baina ya viongozi mbalimbali wa serikali na wafanyabiashara hao, tayari maduka yamefunguliwa na shughuli za kibiashara zinaendelea kama kawaida.
No comments:
Post a Comment