Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Dk. Geofrey Mkamilo (katikati) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Mlingano, Dk. Catherine Senkoro na Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Ilonga Dk. Joel Meliyo kwenye uzinduzi wa Kituo mahili cha usambazaji wa teknolojia za kisasa za kilimo chini ya TARI.
Watalamu wa TARI wakiwa kazini
Na Godwin Myovela
TAASISI ya utafiti wa Kilimo nchini (TARI) imezindua kituo mahiri cha usambazaji wa teknolojia za kisasa za kilimo ambacho kimesheheni wataalamu watakaotoa mafunzo kwa wakulima na huduma za kiugani kwa kipindi chote cha mwaka.
Uzinduzi wa Kituo hicho kilichopo viwanja vya J.K Nyerere Nanenane mkoani Morogoro sasa kinakuwa cha pili kikitanguliwa na kituo kama hicho kilichozinduliwa mapema mwaka jana, eneo la Nyakabindi, Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kituo hicho mkoani Morogoro jana, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geofrey Mkamilo alisema shabaha kubwa ya kituo hicho ni kuongeza tija na uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa wakulima.
"TARI tumejipanga vizuri katika kuleta mageuzi ya kilimo kwa kuhakikisha mkulima analima kisasa kwa kuzingatia kanuni zote za kilimo bora, ndio maana kituo hiki kina wataalamu mbalimbali wa kilimo wakiwemo watafiti," alisema.
Mkamilo alibainisha kuwa azma ya TARI ni kuhakikisha inaendeleza ushirikiano wa karibu na kitaalamu kutoka kwa wadau wengine mbalimbali katika kufanikisha shughuli zake za utafiti kwa lengo la kumsaidia mkulima kuinua tija, kilimo biashara na lishe bora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mathayo Masele, mbali ya kupongeza uwepo wa kituo hicho, aliwakumbusha maafisa ugani kuzingatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa wakati akizindua Kampeni ya Kilimo cha alizeti mkoani Singida hivi karibuni la kumtaka kila afisa kilimo kuwa na shamba la mfano.
"Nitoe wito kwa maafisa ugani tumieni taaluma yenu kwa vitendo kwa kuhamasisha na kisambaza elimu ili kumsaidia mkulima," alisema Masele ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Martin Shigela kwenye tukio hilo.
Meneja wa Mawasiliano ya Habari na Menejimenti ya Maarifa, kutoka Makao Makuu ya TARI Dodoma, Dk. Richard Kasuga alisema uzinduzi mwingine kama huo ambao maandalizi yake yanaendelea unatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Dodoma na Tabora.
"Tunakusudia kuongeza vituo vingine katika maeneo ya Nzuguni Dodoma na Fatma Mwasa Tabora kabla ya kuendelea na maeneo mengine nchi nzima, azma hasa ya TARI ni kuhakikisha tunasambaza teknolojia stahiki za kitafiti kwa tija na ustawi wa kilimo kwa mkulima," alisema Dk. Kasuga
No comments:
Post a Comment