HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 04, 2021

TCAA yazindua Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji Vibali vya Anga kwa Mashirika ya Ndege

 Hussein Ndubikle, Dar es Salaam


Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imezindua Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji Vibali vya anga kwa Mashirika ya Ndege yanayotoka nje ya nchi na yatakayopita anga ya nchini lengo likiwa kuboresha huduma na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Akizindua mfumo huo  jijini Dar es Salaan Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Hamza Johari amesema walishaanza kutumia mfumo wa aina hiyo katika maeneo mengine  na kwamba utatumika kwa ndege zote zinazotoka nje zitakazotumia viwanja vya ndege na zitakazopita anga ya Tanzania.

Amebainisha kuwa mfumo umetengenezwa na watalaamu wa ndani bila gharama yoyote tayari  na umeshaanza kutumika hivyo mteja kokote duniani ataomba kibali kwa njia ya mtandao kwa kuingiza taarifa zake sahihi ndio atapata kibali chake.

Amesisitiza kuwa utoaji vibali hivyo unazilenga Ndege za abiria, zinazohusika na umwagilaji wa dawa za wadudu, utafiti, ndege za kukodi, zinazoleta watalii, matajiri na Wanadiplomasia ambapo zote zitaomba mtandao wa TCAA kwa kujaza taarifa zao shahihi.

Ameongeza kuwa utasaidia kupunguza mlolongo na muda wa uombaji vibali, urahisishaji wa upembuzi wa nyaraka za marubani, kumwezesha mwombaji kujua kiasi cha fedha anachotakiwa kulipia pamoja na mienendo ya huduma za ndege na Mashirika hayo.

Aidha, amesema endapo waombaji vibali watafuata taratibu na sheria zilizowekwa kwa kujaza taarifa sahaihi haitawachukua muda mwingi kwani watapewa ndani ya saa moja au mbili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Uhumi wa TCAA, Daniel Malanga amesema mwombaji atatakiwa kutuma barua pepe kwenda kwa kitengo cha vibali ambapo baada ya kukamilisha atatengenezewa jina  la akaunti yake, jina la kuingilia na namba siri za kuingilia.

Malanga amesema mwombaji wa kibali akishakamilisha hatua za mwanzo atapewa maelekezo ya kujaza taarifa zake sahihi zikiwemo za anga anayotoka, anayopitia, anayoingia, sababu ya kuja nchini, aina ya ndege na usajili wake pamoja na vyeti vya ubora vya Marubani.   

Mkurugenzi huyo amewasisitiza waombaji wote kufuata kanuni na sheria zinazoongoza uombaji vibali kwa kutoa taarifa sahihi ili ziwape urahisi wa kuvipata kwa muda mfupi tofauti na ilivyokuwa awali.


No comments:

Post a Comment

Pages