Sehemu ya Watumishi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL Corporation wakisafisha maeneo mbalimbali ya jiji la Dar Es Salaam ikiwa ni kuadhimisha kilele cha Wiki ya Utumishi kwa Umma leo. |
WAKATI Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi kwa Umma yakifikia kilele chake leo June 23, 2021 Watumishi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL Corporation wamefanya usafi maeneo mbalimbali ya jiji la Dar Es Salaam kitendo walichokiita 'Matembezi ya Usafi' ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo.
Katika matembezi hayo Watumishi wamepita katika maeneo ya Posta Mpya, IFM, Soko la Kimataifa la Feri ambapo pamoja na mambo mengine walikuwa wakiokota taka zote zilizotupwa katika maeneo tajwa na kuyakusanya kwa ajili yakuyapeleka katika maeneo maalum ya kuhifadhi takataka.
Maadhimisho haya ni kwa mujibu wa kalenda ya Umoja wa Afrika (AU) ambapo nchi wanachama huadhimisha kwa kushiriki shughuli mbalimbali zinazohusu Utumishi wa Umma yanaratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Akizungumzia maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Mtahiko Henry amesema Wiki ya Utumishi wa Umma inamkumbusha kila Mtumishi kwamba anawajibika kwa jamii na kumkumbusha kuwa utumishi wake haupaswi kuishia Ofisini bali unaenda mbali zaidi kwa wananchi.
Aidha Mtahiko amesema kupitia matembezi hayo Wananchi watapata fursa kuonana na Watendaji wa TTCL uso kwa uso, na kupata maelezo mbalimbali ya huduma na bidhaa zitolewazo na shirika hilo.
Pamoja na kupata maelezo hayo wananchi pia watapata nafasi ya kutoa maoni kuhusu huduma wanazozipata kutoka katika shirila lao la mawasiliano na kwamba maoni yao yatathaminiwa kwakufanyiwa kazi kwakuhakikisha kero itakayobainika inafanyiwa kazi.
“Sisi ni Watumishi wa Umma kama walivyo watumishi wengine hivyo tunawajibika kwa wananchi na ndiyo maana leo tumefanya shughuli ya kijamii ambapo katika maeneo yote tulipopita tumeahakikisha tunayaacha mazingira yakiwa safi.” Amesema Mtahiko
Ametoa rai kwa Watumishi wote wa TTCL kuhakikisha wanaendelea kuzingatia misingi ya utumishi wa Umma pindi wanapokuwa kazini na baada ya kazi kutokana na ukweli kwamba jamii ndiyo inayowapima tabia na utendaji wao wa kazi.
Katika hatua nyingine Mtahiko amesema TTCL inawatumikia Wananchi kwakuhakikisha inalipa kodi ya kila mwezi kwa wakati ambapo kupitia kodi hizo mwananchi ananufaika kwakupata huduma mbalimbali za jamii ikiwemo maji, barabara, elimu na Afya.
Wiki ya Utumishi wa Umma Barani Afrika ni wiki maalum ya Watumishi wa Umma na taasisi za Umma ambayo husherehekewa kuanzia tarehe 16 Juni hadi 23 Juni kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya Bara la Afrika.
Chimbuko la Sherehe hizi ni uamuzi wa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma uliofanyika Tangiers nchini Morocco mwaka 1994. Uamuzi huu ulizitaka nchi za Afrika kusherehekea sherehe hizo kwa kauli mbiu moja katika Bara zima la Afrika.
Malengo ya msingi ya Wiki ya Utumishi wa Umma Barani Afrika ni pamoja na kuwezesha watumishi wa Umma kutambua Dira, Dhima, na Malengo; Programu na Mikakati; na Mafanikio na Changamoto zinazokabili Utumishi wa Umma, kutambua mchango na umuhimu wa Watumishi wa Umma na umuhimu wao katika kuleta maendeleo nyanja mbalimbali katika Taifa.
Lingine ni kuhamasisha na kuwapa motisha Watumishi wa Umma ili waendelee na kazi yao nzuri ya ujenzi wa Taifa na kuendelea kuwa wabunifu ili kutatua changamoto mbalimbali katika jamii, Kupata mrejesho kutoka kwa wateja na wadau wao juu ya huduma wanazozitoa na Kuwaandaa Watumishi wa Umma ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali.
No comments:
Post a Comment