HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 21, 2021

Anza kuwekeza sasa, jiulize kesho yako itakuwaje


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TUMEZOEA kutafuta pesa, kuzitumia kwa kununua mali ghafi na kuibadilisha kuwa bidhaa ambayo itaenda kukidhi hitaji fulani kwanye jamii.

Kwa mfano, utatumia pesa kununua shamba, unapanda pamba kwenye shamba hilo, ikifikishwa kiwandani itatengeneza shati.

Bei ya shati itakuwa inabeba sehemu ya gharama zote za awali na faida ya muuzaji wa mwisho.

Hili ni jambo jema kwani ndani yake tunatengeneza ajira, tunakidhi hitaji la lazima la mavazi bila kusahau chakula, mambo mengine mbalimbali.

Wakati mwingine badala ya kutumia nguvu kubwa kwa tija ndogo, tunaweza tumia nguvu kidogo muda mchache lakini tukapata pesa nyingi.

Tukiweka nguvu kiasi tukapata tija zaidi, tunakuwa tumeyafanya maisha yawe marahisi na furaha zaidi.

Pia tunakuwa tumeokoa muda mwingi kwa ajili ya shughuli nyingine. Kwa mfano, ukiwekeza fedha kwenye Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja, kazi ya kuwekeza huifanyi wewe, inafanywa na Meneja msisimazi wa mfuko husika. 

Unaweza kuikopesha benki kupitia akaunti ya muda maalumu, kuikopesha serikali kupitia hatifungani.

Hapa ina maana utakuwa unakaa, unafanya shughuli nyingine huku ukisubiria gawio. Kama una gari unaweza lifanya uba kwa kuhakikisha una abiria asubuhi ukienda kazini na ukafanya hivyo wakati wa kurudi jioni.

Pia unaweza kutengeneza tovuti hata ukawa na akaunti kwenye ‘Instagram’, ‘Facebook’ na hata ‘WhatsApp’ ambayo utayatumia kutengeneza fedha.

Kuna shughuli nyingi ambazo sio rasmi ambzzo zinaweza kukuingizia kipato halali. Pia kuna namna nyingi za kupata  pesa bila kutumia muda mwingi katikaajira rasmi.

Unaweza kuwekeza pesa kama pesa bila kukupa pesa au kuitumia pesa yenyewe. Mfano unapoweka pesa kwenye kibubu, chini ya godoro au kuzifukia chini.

Kiasi ulichoweka utakuta kipo hivyo hivyo haijalishi muda, thamani ya ulichokiweka inaweza ikaongezeka, mara nyingi  inapungua, kuna usemi unasema shilingi ya leo sio ya jana.

Ili kukabiliana na thamani kushuka, mfumuko wa bei, kuongeza kipato, tunashauriwa kuwekeza pesa zetu.

Tumezoea kupanda mahindi tuvune, tuuze tupate pesa zaidi (faida); kimsingi ni vizuri kufanya hivyo kwani tunapata faida na chakula kwa ajili ya afya zetu.

Ni vizuri tukajua kama shida ni pesa, tupande pesa kwa maana ya kuwekeza ili tupate pesa zaidi. Mfano, kama utapanda pesa katika uwekezaji wa pamoja, utapanda pamoja na wenzako na kuwa nyingi zaidi.

Mfano, kupitia UTT AMIS, Mfuko wa Ukwasi umeweza kukua zaidi ya mara 2.6 katika muda wa miaka sita. Kama hujaanza kuwekeza, unapoteza thamani katika mali zako.

Pia kumbuka kuwa, hakuna kitu chenye thamani kama muda, unavyochelewa unajirudisha nyuma kimaendeleo.

Kuna msemo wa Kichina unasema wakati mzuri wa kupanda miti ni miaka 20 iliyopita, hili ndio jibu sahihi kwa swali la ni lini nianze kuwekeza?

Muda ni mali, kama ukiwekeza sh. milioni 5, miaka 10 kwa asilimia 15 utapata sh. milioni 22. Pesa hizo kwa asilimia hiyo kwa miaka 15 itakuwa sh. milioni 46.

Kwa haraka utaona pesa uliyoweka miaka 10 kwa asilimia hiyo inakuwa mara 2 tangu uwekezaji miaka 10 hadi 15.

Hii inatokana na uwekezaji unaozingatia faida jumuishi, kadri muda unavyokuwa ndivyo faida inakuwa kwa haraka. Mfano wa sh. milioni tano ni uwekezaji wa mara moja tu.

Tuchukue mfano mwingine ambao utaanza na sh. milioni 5, kila mwezi ukawekeza sh. 200,000 kwa asilimia 14 ndani ya miaka 10 utakuwa na sh. milioni 95.

Pesa hizo hizo zikakaa kwa miaka 20 yaani kwa miaka 10 zaidi utakuwa na sh. milioni 453, zaidi ya nusu bilioni.

Hapa miaka 10,15 na 20 imetumika kama mfano, jambo muhimu uwekezaji unahitaji muda.

Kwa kuzingatia malengo ya mfuko husika muda unaweza ukawa siku, miezi na hata miaka. Hakuna sababu ya mwekezaji mtarajiwa kuwa na hofu.

Angalizo ni kwamba, riba inaweza kupanda au kushuka, pia thamani ya uwekezaji inaweza kupanda au kushuka kutokana na mabadiliko kwenye soko la uwekezaji.

Mabadiliko hayo yanaweza kusababisha ongezeko au upungufu wa riba. Moja kati ya faida kubwa ya kuanza uwekezaji mapema badala ya kusubiri ni kuwahi fursa zinapotokea.

Kwa mfano, thamani ya kipande mfuko mpya unapoanza huwa sh. 100. Baada ya hapo thamani inaanza kupanda hivyo bei ya kukinunua inakuwa juu.

Hali hiyo inatokaana na mwendo wa soko; pia hisa huanza kwa bei ya chini kwa mategemeo kuwa muda unavyokwenda thamani yake inaongezeka.

Ndani ya muda mfupi uwekezaji unaweza ukabadilika kutokana na hali halisi ya kule ambako fedha zako zimewekezwa.

Jambo la msingi ni muda gani utakaa kwenye uwekezaji, si muda gani umeingia sokoni japo kuna mtazamo wa kupanga kustaafu miaka 10 kabla ya muda huo.

Unapofikisha miaka 20 ya kustaafu unaiona mingi lakini ukweli ni kwamba, kila anayekaribia kustaafu atakwambia angependa kuweka mazingira ya kustaafu mapema.

Majuto ni mjukuu, wanasema unapozidi kuchelewa mambo mengi yanatafuna kile ambacho ungeweza wekeza yanajitokeza. Mfano watoto, mikopo, ujenzi, matibabu ya familia, ghrama za maji, uendeshaji nyumba yako.

Ukiwa kijana silaha yako ni muda, tathmini umri wako, muda ambao ungependa kustaafu, tazama vyanzo vya kipato chako, gharama zako, changanua ni kiasi gani unaweza kuweka kando kwa ajili ya kustaafu.

Japo wewe si Mungu, huwezi kujua baada ya kustaafu unaweza kuishi miaka mingapi, ukistaafu ungependa kukakaa wapi?, afya yako na familia kwa ujumla.

Pia fikiria mambo mengine ambayo huwezi yatabiri kama talaka, kifo,watoto. Hakikisha hauna madeni yenye riba au kama yapo unayalipa mapema sana kwani ukidunduliza deni riba nayo inajidunduliza.

Kwa mfano, deni la sh. 100,000 kwa riba ya asilimia 10, litakuwa sh. 110,000, mwisho wa mwaka litakuwa sh. 121,000, mwaka wa pili  litazidi kuwa kubwa.

Unapaswa kuzingatia mambo ya msingi katika kuwekeza, kwanza uwekeze wapi, kwenye hisa,  mikopo au kilimo, majengo au duka.

Kumbuka kwenye kuwekeza kuna sehemu zenye hatari kubwa, hatari za kati na hatari za kawaida. Mwekezaji mwenye umri mdogo anaweza akathubutu kuwekeza maeneo yenye hatari.

Mfano kwenye kuchimba madini, unaweza chimba hadi mwisho wa uhai wako na usipate kitu, hisa unaweza kukaa nazo miaka mingi bila thamani yake kuongeza au zikawa zinapanda na kushuka kila mara.

Kawaidi mwekezaji mwenye umri mkubwa uthubutu wake hupungua hivyo anashauriwa awekeze sehemu zenye ukwasi wa wastani mfano kwenye akaunti za muda maalumu au hati fungani.

Wataalamu wapo hivyo ni vizuri kuwatembelea, mfano UTT AMIS, benki na madalali wa masoko ya hisa.

Pia wataalamu au wafanya biashara maarufu wenye uzoefu wanaweza kuwa msaada sana. Usiingie kwenye chaka usilo lifahamu hivi hivi.

Wataalamu watakutengenezea mseto mzuri, mfano pesa kwa ajili ya malengo ya muda mfupi zinaweza wekezwa sehemu ambazo ni rahisi kuzipata pale mwekezaji anapozitaka kama UTT AMIS, akaunti za muda mfupi  benki, hati fungani za muda mfupi za serikali.

Kwa malengo ya muda mrefu zinawezwa wekezwa katika  hati fungani za muda mrefu za serikali au kampuni binafsi.

Uwekezaji kwenye sehemu ambazo ni za muda mrefu zinatoa fursa ya uwekezaji wako kukua (unakuza uwekezaji).

Kumbuka uwekezaji unaolipa sana unaambatana na hatari kubwa kuliko uwekezaji  unao lipa kidogo.

Kwa maneno mengine, pale kwenye hatari sana kuna uwezekano mkubwa wa kupata faida kubwa lakini upande wa pili wa shilingi pia kuna  uwezekano wa kupata hasara.

Uvumilivu wako dhidi ya changamoto katika uwekezaji ni muhimu sana, si rahisi meli ya uwekezaji ikaenda shwari kila siku.

Wakati mwingine itabidi ubadili mseto wako wa uwekezaji kama kuhamisha kiasi au uwekezaji wote kutoka kwenye hati fungani kwenda kwenye hisa au tofauti yake.

Jipime uwezo wako wa kustahimili hasara, ukiona uthubutu wako ni mdogo chagua sehemu ambazo viashiria hatarishi ni vichache, mfano bondi za serikali,  akaunti za muda maalumu.

Itakuwaje kama kipato chako ni finyu? Unaweza ukajikuta bado unaendelea kufanya kazi baada ya kustaafu kwa sababu kipato chako ni kidogo.

Kumbuka pesa unazowekeza kwa ajili ya kustaafu na matumizi yako ya kila siku vina athari kwenye kipato kinachobaki kwa ajili ya matumizi mengine.

Ili uweze kuongeza uwekezaji wako jambo la msingi kwanza punguza madeni, unatakiwa ukope kama inabidi tu, ukizoea kukopa inakuwa kama ugonjwa.

Ni kama vile wasemavyo Waswahili kama tatizo ni msumari na suluhisho ni nyundo basi kazi yako itakuwa kutatua tatizo kwa kuugonga msumari tu kumbe kuna namna nyingi za kutatua tatizo.

Badili tabia ya matumizi, jaribu kupunguza matumizi kwenye anasa mbali mbali na yale yasiyo ya lazima.

Fikiria kuwa na nyumba ndogo, gari ya bei ndogo, badili tabia, mtazamo uwe kesho yako itakuwaje?

Utaahirisha matumizi fulani kwa sasa kwa ajili ya uhakika wa maisha ya badae. Panga matumizi kila mwezi, zingatia bili muhimu kama maji, umeme, gesi, kodi, afya, chakula, pia unaweza kukadiria burudani kwa kiasi cha chini kabisa.

Tathimini mapato tarajiwa kutoka katika pensheni na kiasi ulichoweka kwa ajili ya kustaafu.

Japo ni ngumu jaribu kutathimini utaishi miaka mingapi, hapa unaweza fanya tathimini ya afya yako, mfano kama una maradhi yanakusumbua ya aina gani.

Pengine katika ukoo wenu wengi wanakufa wakiwa na umri gani, kwa maradhi gani, afya yako ikoje, hatari gani ambazo hukumbana nazo kila siku, zinaweza dhuru maisha yako?.

Jifunze bajeti, jaribu kuangalia kama mapato yatazidi matumizi, hii ina maana faida au matumizi yatakuwa sawa na mapato, hapa maana yake hakuna faida wala hasara.

Mapato yanapokuwa madogo kuliko matumizi ni hasara hivyo ni muhimu kuangalia gharama zisizidi mapato. Ili  kulijua hili si lazima uwe mwalimu wa hesabu.

Unapaswa kujua pesa zako zinakwenda wapi na kwanini ziende huko. Kuwekeza kwa ajili ya kesho ni muhimu. Unaweza kupoteza kazi au kampuni kufilisika, maradhi yanaweza kukutoa kwenye ajira,.

Mambo kama haya na mengine mengi yanakulazimu uweke akiba. Akiba nzuri ni ile iliyowekezwa sehemu yenye kuiwezesha ikuwe.

Kumbuka kubana matumizi sio kushinda njaa au kushindwa kukutana na wenzako katika jambo fulani ikiwemo buruduni.

Jambo la muhimu ni kutenga kiasi fulani kwa baadae yako sambamba na kufanya matumizi sahihi. Kuna wale ambao husema sihitaji nyumba kubwa au gari kubwa.

Sitaki makuu, mawazo kama haya yanaweza kuwa chanzo cha uzembe na kupunguza nguvu zako za kusukuma maisha ili ufikie hatua ya juu kabisa.

Muhimu ni kuwekeza kwa juhudi zote. Mfano badala ya kwenda GYM kufanya mazoezi, fanya mazoezi nyumbani, badala ya kwenda hoteli kunywa kahawa, kunywa kahawa nyumbani, kiasi unachookoa kiwekeze UTT AMIS.

Serekali ilianzisha kampuni hii ili wananchi wawe na sehemu inayozingatia usalama, kupata faida nzuru huku ukiendelea na shunghuli nyingine.

Tunasema wekeza bila ‘stress’, funga mkanda ili baadae uishi vizuri; kila siku jaribu njia mpya za kukuza kipato, epuka madeni yasiyo ya lazima, usilimbikize madeni, panga matumizi na fuata mpango wako.

Mifuko ya uwekezaji ya pamoja ni chombo cha uwekezaji kinachokusanya pesa kutoka kwa watu, kampuni ili kupata mtaji mkubwa, mara nyingi huwekezwa kwenye kampuni zilizo chini ya Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

Upande mwingine fedha hizo huwekezwa maeneo ya kukopesha kama akaunti za muda maalumu benki, hati fungani (mkataba maalumu wa mkopo wa serikali au kampuni binafsi). Hati fungani zipo za muda mfupi, mrefu.

Benki kuna bidhaa mbalimbali za kifedha zinazohusisha kukopeshana kwa masharti maalumu kama riba na muda wa mkopo.

Ukiondoa hisa, pesa nyingi za uwekezaji huwekezwa kwenye mikopo yenye mkataba maalumu ambapo hatari ya kupotea ni ndogo sana.

Mfano, mikopo kwa serikali ambayo kwa kawaida haina hatari au kama zipo ni kidogo, mara nyingi huwa zilizo nje ya uwezo wa binadamu.

Kila mfuko unaosimamiwa na UTT AMIS una kanuni mbalimbali ambazo zimeainishwa kwenye waraka wa makubaliano.

Ni wajibu wa mwekezaji kusoma kanuni za mfuko na kuzielewa ili ajue haki zake, tahadhari gani achukuwe kabla ya kuwekeza. Pesa zinasimamiwa na Meneja, walio kusanya wanaendelea na shughuri zao nyingine.

Meneja anawekeza kwa niaba yao chini ya masharti husika, pia Meneja anazitawanya hizo pesa kitaalamu, ananunua hisa mbalimbali, hati fungani.

Pia anakopesha kwa benki mbalimbali faida inayopatikana ni ya wawekezaji, Meneja anatoza tozo ya usimamizi. Pesa za mwekezaji zinagawiwa katika vipande.

Viipande ni kama hisa, mwekezaji akitaka kukuza uwekezaji wake ananunua vipande zaidi, akitaka pesa zake anauza vipande vyake.

Thamani ya vipande hupanda na kushuka kutokana na marejesho ya kule Meneja alipowekeza. Meneja ni lazima anunue vipande pale mwekezaji anapotaka kuuza.

Pia lazima auze vipande mnunuaji anapotaka kununua, haya masharti ni ya msingi, yapo kwenye waraka wa makubaliano, vinginevyo mwekezaji ana haki ya kuchukua hatua.

Faida za uwekezaji wa pamoja, Meneja anawekeza sehemu mbalimbali, haweki mayai yote sehemu moja. Hii ina maana kuwa kama sehemu moja hailipi itafidiwa na sehemu nyingine zinazolipa.

Kidole kimoja hakivunji chawa, mkikusanya pesa pamoja mnakusanya mtaji mkubwa ambao utakuwezesha kufanya biashara ambayo ungekuwa mwenyewe usingeifanya.

Pia wingi wa pesa unaongeza nguvu ya majadiliano, mwenye kisu ndiye anayekula nyama. Ni rahisi mifuko ya uwekezaji mfano UTT AMIS, mwekezaji anaweza anza kuwekeza kwa sh. 10,000 tu.

Huitaji fremu, leseni ya biashara, kijana wa kukusaidia kuuza, muda unautumia kwa mambo mengine ya tija.

Pia una chaguo la kupokea gawio au kukuza mtaji, yote ni uamuzi wako.Pia kuna unafuu kwenye gharama.

Mfuko unapokuwa na pesa nyingi manunuzi yanakuwa na punguzo kama ilivyo kwenye duka la jumla, kawaida duka la jumla bei huwa ni tofauti na duka la rejereja.

Kwa sababu wawekezaji ni wengi ina maana gharama kwa kichwa zinapungua pia, yaani gharama zinabebwa ki umoja tofauti na mwekezaji anapofanya mwenyewe.

Meneja wa mifuko anakuwa na wataalamu waliobobea ambao kila siku hufuatilia taarifa za soko. Wataalam hao huangalia mambo mbalimbali, wanafanya upembuzi yakinifu kabla ya kuwekeza mahali popote.

Kwa mfano, kabla ya kununua hisa za kampuni fulani, wataangalia historia ya kampuni hiyo, uwezo wa kifedha, ushindani, uongozi, uchumi, masoko kiujumla, matarajio ya baadae na mambo mengine kadhaa.

Pamoja na faida nyingi, uwekezaji wa pamoja kama uwekezaji mwingine kuna wakati unakumbana na changamoto.

Kati ya changamoto kubwa ni kutoweza kumuhakikishia mwekezaji kupata asilimia fulani kila mwaka, hii inatokana na ukweli kuwa faida inategemea rejesho la kule alikowekeza Meneja.

Kama Meneja kawekeza kwenye hisa, mwaka huu zinaweza zikalipa sana kuliko mwaka unaofatia, hii ina maana ya kuwa mavuno yatakuwa tofauti.

Pia benki zinakuwa na riba tofauti, kipato cha mwekezaji kitakuwa kinapanda au kushuka kutokana na rejesho la kule Meneja anapowekeza.

Changamoto nyingine, maeneo ya uwekezaji yameainishwa kwenye mkataba hivyo kwa namna yeyote Meneja hatakiwi kuwekeza kwenye maeneo zaidi ya yale yaliyotajwa.

Hii ina mnyima Meneja uwezo wa kuwekeza kama itatokea fursa ambayo ni dhahiri ingeweza kuleta faida.

Pia Meneja ni binadamu asipoangaliwa vizuri anaweza kuingiza matakwa yake binafsi ndiyo maana uwekezaji wa pamoja unasimamiwa na Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) kwa Tanzania.

Meneja anaweza wekeza sehemu kwa nia njema lakini kukawa na mabadiliko ambayo si mazuri ki uwekezaji sokoni.

Wakati mwingine kwenye masoko panaweza kutokea majanga mbalimbali, mfano Covid-19, mafuriko, tetemeko la ardhi, pia soko linaweza kukumbwa na mfumuko wa bei, kupungua thamani ya fedha, mambo mengine mengi tu.

Katika hali, mwekezaji anashauriwa kuwa na subira kwani hakuna hali ya kudumu, muda unavyokwenda pamoja na juhudi za Meneja, jitihada za wadau wote kwa vile janga linamkumba kila mtu.

Meneja pia anatakiwa akwepe kuwekeza sehemu moja, mfano kununua hisa nyingi za kampuni moja hatakama hiyo kampuni inafanya vizuri kiasi gani.

Ipo siku mambo yatakuwa si shwari hivyo ikaleta shida kwani itakuwa kama vumeweka mayai yote kwenye kapu moja, likianguka mayai yote yanavunjika.

Riba inaweza kuwa changamoto, wakati mwingine zinaenda juu au chini, riba ni gharama ya mkopo, ikiwa juu wakopaji wanapungua na ikiwa chini wanaongezeka. Riba inaendana na mahitaji na uwepo wa fedha.

Hatari nyingine inawezekana Meneja sio mwangalifu, hana ukwasi wa kutosha wa kulipa wawekezaji wanapohitaji pesa zao. Ili kukabiliana na hili, utaalamu mkubwa hutumika kuhakikisha fedha zinawekezwa sehemu ambayo uwekezaji unawiva mara kwa mara ndani ya muda mfupi.

Pia kuwa na fungu ambalo malipo yakihitajika Meneja anaweza kuchukua ndani ya muda mfupi, kulipa mara moja kwa mujibu wa misingi husika.

Kama ilivyoelezwa hapo mwanzo kiasi kidogo huwekezwa kwa kampuni binafsi ambazo zimefanyiwa upembuzi wa kutosha, katika hali ambayo si ya kawaida kampuni binafsi inaweza kuchukua mkopo na kushindwa kulipa.

Uwekezaji anuai utasaidia kupunguza hatari hii, mkataba wa mkopo utaeleza kama mkopaji ameshindwa kulipa inakuwaje.

Hatari nyingine ni za kawaida kama za kisiasa, kiuchumi, mfano nchi nyingine mapinduzi kila siku, pia kuna hatari nyingine zinakuwa za kidunia mfano uchumi wa nchi kubwa ukiyumba kishindo chake kinasambaa hadi kwa nchi ndogo kiuchumi, vita kila siku, mfumuko wa bei, kushuka thamani ya fedha, mambo mengine.

Ni vizuri mwekezaji asome waraka wa mfuko, aelewe vizuri, aongee na wataalamu wabobezi, pia sio mbaya kuangalia wamiliki wa kampuni, historia yake.

Mabadiliko ya kodi nayo yanaweza kuufanya uwekezaji ukawa wa kuvutia na rahisi au ukawa wenye kukatisha tamaa na mgumu.

Kodi ni gharama kwenye uwekezaji, zikiwa ndogo zinavutia wawekezaji na zinafanya mazingira yawe rafiki. Tumeona faida na hasara za uwekezaji wa pamoja, tumeona ni jinsi gani tunaweza kuongeza kipato cha kila siku.

Tumeitambua UTT AMIS kama ni kampuni ya Serekali iliyo chini ya Wizara ya  Fedha na Mipango ikiwa imepewa dhamana ya kusimamia mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Hadi sasa mifuko hiyo iko sita ambayo ni Mfuko wa Umoja, Watoto, Wekeza Maisha, Jikimu, Ukwasi na Hati Fungani. Historia ya mifuko yote imekuwa ni hadithi nzuri kwa wawekezaji wote wa kipindi cha kati na kirefu.

Hayupo hata mmoja aliyepata hasara, leo hii mifuko hii imekuwa chaguo na kimbilio la Watanzania wengi.

Tukumbuke kuwa, thamani ya kipande inaweza kupanda au kushuk kwa kila uwekezaji, hakuna uwekezaji ambao utakupa faida sawa kila wakati.

Kumbuka kuna namna tatu za kupata pesa kwenye uwekezaji wa pamoja, kwanza unaweza chagua kupata gawio ambalo litatokana na faida itokayo kwa Meneja anapowekeza.

Pili faida inayoongeza thamani ya mtaji, mtaji utaongezeka kwa kasi kama huchukuwi gawio maana gawio linakuwa sehemu ya uwekezaji.

Kama unachukua gawio bado mtaji utaongezeka lakini kwa kiasi kidogo. Faida inatokana na ongezeko la thamani ya vipande, thamani inaongezeka kutokana na mchango wa faida inayotokana na uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

Pages