HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 26, 2021

MAKAMU WA RAIS AWEKA JIWE LA MSINGI HOSPITALI YA KANDA YA KUSINI

 

Makamu wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango  akizungumza na wananchi waliojitokeza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini, Mtwara iliopo Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara. (Picha na VPO).


Makamu wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango  akiweka jiwe la msingi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini iliopo Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara, Julai 26,2021.

 

Na Mwandishi Wetu

 

Makamu wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango, leo Julai 26, 2021 ameweka jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliopo  Mikindani Mkoa wa Mtwara. Hospitali hiyo inatarajiwa kuhudumia mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.   Ujenzi wa Hospitali hiyo unagharimu shilingi bilioni 15.8.

 

Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali, zahanati na vituo vya afya katika mkoa wa Mtwara ili kuwasogezea huduma za afya wananchi  ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa madawa, vifaa tiba na vitendanishi.

 

Aidha amesema serikali itaendelea kuajiri watumishi wa sekta ya afya na sekta nyingine na kuutaka uongozi wa Mkoa wa Mtwara  kuimarisha utaratibu wa utoaji dawa na kuhakikisha hakuna upotevu wa dawa. Amesema Serikali itachukua hatua kali kwa yeyote atakayefanya uzembe au kuhusika na wizi wa dawa hizo ikiwemo kutaifishwa kwa mali za yeyote atakayehusika katika wizi huo.

 

Makamu wa Rais ametoa wito kwa taasisi za serikali zinazotekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali kuendelea kuwatumia Shirika la Nyumba la Taifa pamoja na malighafi zinazokidhi viwango kutoka nchini Tanzania kama ilivyofanyika katika ujenzi wa Hospitali hiyo.

 

Akiwa Hospitalini hapo Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Mtwara kwa juhudi zao za  kutunza mazingira ambao kuanzia mwaka 2021 uanze, wamepanda miti ya kawaida 4,480,600 kati ya hiyo, miti 4,312,74,3 imestawi.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amesema tayari Wizara ya Afya imepata kibali cha kuajiri watumishi mia tatu kwaajili ya Hospitali hiyo inayotarajiwa kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi Oktoba.

No comments:

Post a Comment

Pages