Dkt. Herbert Makoye Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) akimkabidhi Cheti cha shukrani Bi. Mwanaidi Adinan Msuya (Dj Sweetlady) kutoka Peramiho DJ's aliyekipokea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Peramiho wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa vya kufundishia vilivyotolewa na umoja huo.
Na Andrew Chale, Bagamoyo
WADAU mbalimbali wa ndani wamejitokeza kusaidia maendeleao ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa kuipatia msaada wa vifaa mbalimbali vya muziki kwa ajili ya kufundishia huku vifaa hivyo vikitajwa kuwa ni chachu katika kukuza Sanaa chuoni hapo.
Akizungumza mapema leo katika hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo kutoka kwa wadao hao wakiwemo Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi, Peramiho Dj's na ABC Foundation, Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Hubert Makoye, alisema msaada huo uliotolewa na watanzania ni chachu kwao kuondoa mazoea ya kuwategemea wafadhili wa nje.
"Msaada huu wa busta, drum za muziki, jezi za mpira na ukarabati wa kiwanja cha mpira wa kikapu, unatuonesha kwamba tuna nafasi ya kuwapata wafadhili ndani ya nchi kuliko kuwategemea wafadhili wa nje.
Tukifungua macho taasisi binafsi na watu mmoja mmoja wananafasi kubwa ya kutupatia msaada," alisema Makoye.
Aliongeza kuwa,TaSUBa inawahudumia wananchi hivyo lazima waimarishe mahusiano na jamii.
Dkt. Makoye alisema licha ya msaada huo, TaSUBa inakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kufundishia huku miundombinu ikiwa chakavu.
Kwa upande wake mwakilishi wa Peramiho Djs, ambao wametoa msaada wa busta ya muziki, Bw. Ricardo Sisco, alisema wamevutiwa kutoa msaada huo ili kuendeleza vipaji vya vijana katika Sanaa.
"Sanaa ni ajira, tumejiajiri kupitia sanaa, tulipata fursa ya kusherehesha UMISETA na UMITASHUMTA hivyo wasanii wasingekuwepo tusingepata fursa, tunawaendeleza wasanii ili kuinua ajira yetu," alisema Ricardo Sisco.
Kwa upande wake Mariam Mkuki, aliyemwakilisha Bw. Aboubakari Mlawa ambae ni Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Bagamoyo ambae ametoa dramu za muziki pamoja na jezi kwa timu ya TaSUBa, amesema wao ni wadau wakubwa wa Sanaa na wataendelea kusaidia kukuza Sanaa nchini kwa kuwa lengo ni kuikuza na kuiboresha Sanaa ya Tanzania.
Naye Aziza Simba, mwakilishi wa ABC Foundation ambao wamefanya ukarabati wa kiwanja cha mpira wa kikapu alisema msaada huo umetokana na mapenzi makubwa ya sanaa waliyonayo na kuahidi kuendelea kudumisha mashiriano baina yao na TaSUBa.
No comments:
Post a Comment