Mratibu wa Mradi wa Tajirika na Kilimo kutoka Shirika la CARE Bw. Samuel Chambi akisisitiza jambo kwa watekelezaji wa Mradi huo wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tajirika na Kilimo kilichofanyika jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23 Julai 2021.
Na Mwandishi Wetu
WAKULIMA
2,176 wa mkoa wa Morogoro, Iringa na Jombe wamenufaika na mafunzo ya
stadi katika kilimo na ufugaji yaliyotolewa kupitia mradi wa Tajirika
na Kilimo unaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi
(VETA), Shirika la Kimataifa la CARE na Taasisi ya Ukuzaji Kilimo Uwanda
wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Akizungumza wakati wa kikao
cha tathmini ya utekelezaji wa mradi jijini Dodoma, Mratibu wa Mradi huo
kutoka VETA, Perecy Ugula, alisema wakulima hao walipatiwa mafunzo ya
ufugaji bora wa mifugo hasa ng’ombe wa maziwa na kuku, kilimo cha mazao
mchanganyiko, kilimo cha mbogamboga na matunda.
Ugula alisema mafunzo hayo yamefanikiwa kubadili uendeshaji wa shughuli zao hizo kuwa za kisasa na za kibiashara.
"Wakulima
2,176 wanawake 1,294 na wanaume 882) wa mikoa ya Morogoro, Iringa na
Njombe wamepata mafunzo ya ufugaji na kilimo bora kupitia Mradi wa
Tajirika na Kilimo," alisema.
Ugula, alitaja mafanikio mengine
yaliyopatikana kwenye mradi huo ni pamoja na uandaaji wa mitaala miwili
ya sekta ya kilimo, ambayo ni Mtaala wa Kilimo cha Mbogamboga na
Matunda, Mtaala wa Kilimo cha Mazao na kuuboresha mtaala wa Afya na
Ufugaji wa Mifugo.
Kwa upande wake, Afisa Tathmini na
Ufuatiliaji wa Shirika la Kimataifa la CARE, Edwin Sallu, alisema
kupitia utekelezaji wa mradi huo wamegundua uwepo wa uhitaji mkubwa wa
mafunzo ya stadi za kuboresha shughuli za kilimo kwa wakulima
wadogowadogo vijijini na kwamba wengi wao wako tayari kugharamia mafunzo
hayo kama inavyofanyika sasa katika Mradi wa Tajirika na Kilimo.
Ofisa huyo, ameiomba VETA kupanua zaidi wigo wa mafunzo kwa mfumo wa kuwafuata wahusika katika maeneo yao vijijini.
Sallu
alisema mafunzo hayo yamewezesha kuunda vikundi 141 vya uzalishaji
katika sekta ya kilimo cha mazao mchanganyiko, mbogamboga na matunda na
ufugaji wa kibiashara, ambapo kwa sasa wanafanya shughuli zao za kilimo
kwa umoja.
Pia alisema kwa sasa uzalishaji mazao kwa sasa
yanapatikana kwa wingi, ubora na uhakika wa kufikia masoko ya bidhaa zao
na kuwezesha wakulima hao kukopesheka kwa urahisi na kupata faida
nzuri.
“Kwa kweli tumeshuhudia manufaa makubwa ya mafunzo
yaliyotolewa kupitia mradi huu kwa wakulima vijijini, hasa ukizingatia
kuwa asilimia 67 ya wanufaika ni wanawake na watoto wa kike ambao
tunaamini wataleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao,” amesema.
Meneja
wa Kongani ya Kilombero kutoka Taasisi ya SAGCOT, John Nakei, alisema
Taasisi yake itaendelea kutoa ushauri, kuwaunganisha na fursa za masoko,
na kutoa elimu zaidi kwa wakulima katika mikoa hiyo ili kuwasaidia
kuendesha shughuli hizo za kilimo kwa tija zaidi na kuwezesha uzalishaji
endelevu wa chakula.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa
Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Kejeri Gillah,
licha ya kuwapongeza wadau katika utekelezaji wa mradi huo, ameshauri
kuweka mkakati wa uendelezaji wa shughuli zilizofanywa kwenye mradi huo
ili wakulima wengi zaidi wanufaike na mafunzo hayo.
Mkurugenzi
wa VETA Kanda ya Nyanda za Juu, Susan Magani, alisema VETA inaendelea na
jitihada mbalimbali za kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanawafikia
wananchi wengi zaidi, hasa maeneo ya vijijini, na kwamba anaamini kuwa
wakulima wengi zaidi nchini watanufaika na mafunzo hayo ili kuboresha
shughuli zao.
Mradi wa Tajirika na Kilimo ulianza kutekelezwa
mwaka 2018 kwa lengo la kujenga na kuimarisha ujuzi katika sekta ya
kilimo kwa wakulima 2,200 na unatarajiwa kumalizika Desemba 2021.
No comments:
Post a Comment