HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 27, 2021

TCU yapongezwa kwa kusimamia taasisi za elimu ya juu kwa weledi

 


Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, akifafanua jambo kwa mgeni rasmi Katibu wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said (wa pili kushoto), alipotembelea banda la tume hiyo katika Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Afisa Uthibiti Ubora Mwandamizi wa TCU, Hilder Kawiche (kushoto), akitoa maelezo kwa mgeni rasmi, Katibu wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said wakati alipotembelea banda lao.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, akimuongoza mgeni rasmi kutembelea mabanda ya washiriki wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia. 
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
  Katibu wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, akifungua rasmi Maonyesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam,
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa vyuo vya nje.
 
Baadhi ya wadau wakiwa katika maonesho hayo.

 
Wakuu wa taasisi mbalimbali wakiwa katika hafla ya uzinduzi huo.
 
 
Na Upendo Kombe, Dar es Salaam

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imepongezwa kwa kusimamia taasisi zinazotoa elimu ya juu kwa weledi na kutoa rasilimali watu ambao wanaisaidia serikali kuleta tija katika sekta mbalimbali nchini. 

 

Akizungumza leo katika ufunguzi wa Maonyesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, Katibu wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, amesema tume hiyo imefanya kazi kubwa kwa kuandaa maonesho hayo ambayo yanatoa fursa kwa washiriki mbalimbali kuonyesha huduma mbalimbali zinazohusiana na taasisi zao.

 

Zena amesema “Tume ya Vyuo Vikuu imekuwa na mchango mkubwa katika Elimu ya Juu katika kusimamia ubora wa taasisi zote zinazotoa elimu ya juu nchini.”

 

Amesema katika kuinua Uchumi wa Nchi Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ina jukumu kubwa la kutengeneza rasilimali watu ambao watasaidia katika kukuza viwanda na kuishauri Serikali katika mambo mbalimbali ambayo yana tija kwenye Taifa.

 

“Maonyesho yana umuhimu mkubwa kwakuwa yanatoa Fursa kwa Taasisi mbalimbali kujitangaza na kuonyesha huduma wanazozitoa pamoja na kufafanua tija zinazopatikana kwa mtu mmoja mmoja, Jamii pamoja na Taifa kiujumla.

 

Pia ameelezea kwa upande wa wanafunzi ni fursa nzuri ya kuongea na wahadhiri wenye weledi na kufanya mwanafunzi afanye maamuzi ambayo ni sahihi baada ya kuhitimu Elimu ya Sekondari”. Amesema Zena

 

Licha ya hayo amekiri kufurahishwa na kazi nzuri inayofanyika katika mabanda ambayo yameshiriki katika maonesho haya ambapo amejionea wananchi wakipewa Elimu na kuelezewa fursa mbalimbali zinazopatikana katika taasisi hizo.

 

Naye Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Prof. Charles Kihampa amesema maonyesho ya mwaka huu yana lengo la kutoa fursa kwa taasisi zinazoshiriki kujitangaza pamoja na kuonyesha huduma zao na mchango wao katika Serikali kupitia Elimu ya juu Sayansi na Teknolojia.

 

“Maonyesho haya yanawapa nafasi pia wale ambao wanampango wa kujiunga na Elimu ya juu kufanya maamuzi sahihi  ya udahili baada ya kujionea mafunzo yanayotolewa katika vyuo mbalimbali”Alisema Kihampa.

 

Kihampa ameongeza kuwa mwaka huu jumla ya Taasisi 75 zimeshiriki kulinganishwa na Taasisi 65 zilizoshiriki katika maonyesho ya 15 mwaka jana 2020, Taasisi zinazotota mafunzo kwa ngazi ya Elimu ya juu ziko 54, Mabaraza ya uthibiti wa ubora 2 (NACTE, TCU).

 

Wakala wa Taasisi za Serikali 5, Bodi za usajili wa Wataalamu 3, Taasisi za Sayansi, Teknolojia na Utafiti 1, Huduma za kifedha 1 na Wakala wa vyuo vikuu vya nje 8.

  

Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia , Prof. James Mdoe amewataka wanafunzi kujiandaa vizuri pindi wanapokuwa shuleni na pia kutumia maonesho haya vizuri kujifunza ili kuchagua kilichobora.

 

Maonyesho hayo yalianza Julai 26 na kufikia kilele chake Julai 31, 2021 yamehudhuriwa na wadau wa Elimu, Wataalamu wa Sayansi na Teknolojia, Wasanii, Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi.

No comments:

Post a Comment

Pages