HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 15, 2021

WATEJA SABASABA WAVUTIWA NA SIMU ZA MEZANI BILA WAYA ZA TTCL


 Meneja wa Banda la TTCL, Ramadhani Mshana (kulia) akimkabidhi simu Kaimu Meneja wa Utafiti na Mipango wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. John Fwalo mara baada ya kununua ndani ya banda la TTCL.


Sehemu ya wateja wakipata maelezo kuhusiana na bidhaa mpya za simu za mezani zinazofanya kazi bila waya (FWT - wireless) ndani ya Banda la TTCL kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 45 yaliyomalizika hivi karibuni Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

 

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepata mafanikio makubwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 45 ya sabasaba 2021, yaliomalizika juzi jijini Dar es Salaam, ambapo bidhaa zake mpya za simu za mezani zinazofanya kazi bila waya (FWT - wireless) zimekuwa kivutio kikubwa na kununuliwa kwa wingi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Meneja wa Banda la TTCL Sabasaba, Ramadhani Mshana alisema kulikuwa na mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo ya 'FWT - Wireless' kwa wateja waliofika katika banda la TTCL kwenye maonesho ya Sabasaba kiasi ambacho mzigo wa bidhaa hiyo uliisha.

"Mzigo wote ulioletwa katika maonesho ulimalizika kabla ya siku ya kilele cha maonesho na kutulazimu kuagiza mzigo mwingine ambao nao pia uliisha kabla ya kumalizika kwa maonesho. Kiujumla  TTCL imepata mafanikio makubwa katika uuzaji wa bidhaa zake pamoja na huduma kwenye maonesho haya," alisema  Meneja Mshana.

Aliongeza kuwa bidhaa zingine zilizopata mahitaji makubwa ni vifaa vya 'wireless internet' kama 'Mifi', Wingle pamoja na 'Router' na hii ni kutokana na ongezeko kubwa la matumizi ya internet kwa wananchi.

Aidha bidhaa nyingine iliokuwa kivutio banda la TTCL ni 'N-Card' ambayo awali watu wengi hawakuwa na uelewa wa matumizi ya card hiyo, wakidhani ni kwa ajili ya kulipia viingilio katika mechi za mpira pekee. Lakini baada ya kupatiwa ufafanuzi wa matumizi yake na mategemeo ya matumizi yake katika siku za mbeleni, manunuzi ya kadi hiyo yaliongezeka zaidi.

"Kwa upande wa huduma biashara ya Call Center (Call Center Business), imekuwa na mapokeo ya kipekee na maombi ya kupatiwa huduma hii yalijitokeza kutoka taasisi za umma na binafsi. Huduma hii ambayo tunaweza kuitoa kwa taasisi za ndani na hata za kimataifa imeonekana ni mkombozi kwa taasisi mbalimbali ambao hawakuwa na ufahamu wa hili," alisema Bw. Mshana.

"Mfano kuna makampuni makubwa ya Marekani na Ulaya, lakini Call Center zake zipo India, Indonessia, Malaysia na Philipines. TTCL kwa sasa inaweza kutoa huduma hii kwa makampuni na taasisi za ndani na nje kama Rwanda, Kenya, Uganda na nchi nyingine yoyote, Gharama yetu ni ndogo sana."

Hata hivyo alisema huduma na bidhaa zilizotolewa kwenye maonesho ya Sabasaba kuwakumbusha kuwa hauduma bora na bidhaa hazijaishia sabasaba, kwani zitaendelea kutolewa kwenye maduka na ofisi za TTCL zilizoko maeneo mbalimbali hivyo wananchi kuendelea kujipatia. "Mtuite tutakuja au temembelea vituo vyetu vya huduma kwa wateja tutakuhudumia kwa wakati," alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

Pages