Ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba wakiimba wimbo wa Taifa wa Msumbiji kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Mawaziri wanaohusika na masuala ya Fedha na Uwekezaji wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jopo la Mapitio ya Uchumi Mpana (Peer Review Panel), uliofanyika kwa njia ya mtandao katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Mhe. William Ole Nasha na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban.
Na Josephine Majura, Dar es Salaam
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), imeipatia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiasi cha Dola Milioni sita kwa ajili ya kugharamia ufanyaji upembuzi yakinifu wa mradi wa reli ya Mtwara mpaka Mbambabay.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Mhe. Jamal Kassim Ali wakati wa Mkutano wa Mawaziri wanaohusika na masuala ya Fedha na Uwekezaji wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jopo la Mapitio ya Uchumi Mpana (Peer Review Panel), kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, uliofanyika kwa njia ya mtandao katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Ali aliongeza kuwa upembuzi huo ukikamilika utawezesha upatikanaji wa wakandarasi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli hiyo ambayo kukamilika kwake kutasaidia kukuza uchumi na biashara katika Ukanda wa Kusini hususan mikoa ya Lindi, Mtawara na Rukwa.
“Kupitia mikutano huu tumeweza kuchangia mawazo na ushauri mbalimbali ili kusaidia nchi zetu katika kukuza biashara na uchumi kwa ujumla katika nchi wanachama wa SADC pamoja na kujadili uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo wa SADC utakaosaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizi, alisisitiza Mhe. Ali.
“Tanzania tumekuwa vinara katika ukombozi wa kisiasa kwa nchi wanachama wa SADC, sasa tumeona tuwe vinara pia katika masuala ya kiuchumi ndiyo maana tumeona tulizungumzie hili pia la uanzishwaji wa mfuko huo”, alisisitiza Mhe. Ali.
Alifafanua kuwa ni vema nchi wanachama wa SADC kwa umoja wao washikane mikono kuhakikisha mfuko huo muhimu wa maendeleo unaanzishwa ili kurahihisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Aidha, Mhe Ali aliongeza kuwa kutokana na changamoto ya Uviko- 19 nchi nyingi zimeathirika kiuchumi, hivyo aliiomba nchi ya Afrika Kusini kutumia Jumuiya ya Nchi zenye uchumi mkubwa Dunia (G20) ikiwemo Korea, China kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika kipindi hiki cha Uviko- 19.
“Kuna haja sasa ya kutumia chombo hiki cha Kikanda cha SADC kuainisha changamoto tunazokutana nazo hivyo tunaiomba Afrika Kusini kuzisema changamoto hizi kwenye vikao vya Jumuiya ya G20 kwa kuwa ni nchi wanachama,” alisisitiza Mhe. Ali.
Alisema kutokana na changamoto ya Uviko – 19 nchi nyingi zimekumbana na changamoto ya ongezeko la kodi na riba kwenye mikopo waliyopata kutoka Washirika wa Maendeleo hivyo kuathiri uchumi wa nchi hizo.
Mhe. Ali, aliipongeza Sekretarieti ya SADC, Wajumbe wa Kamati ya Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi wa Fedha na Uwekezaji na Benki Kuu wa Jumuiya ya SADC kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa siku tatu kuandaa na kuchambua masuala muhimu ya mkutano huu na kurahisisha kazi ya Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji pamoja na Jopo la Uchumi Mpana.
Mkutano wa SADC kwa njia ya mtandao ulifanyika chini ya Mwenyekiti ambaye ni Waziri wa Uchumi na Fedha wa Msumbiji Mhe. Adriano Afonso Maleiane, tarehe 15 Julai, 2021 kutokea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es salaam, ambapo ulitanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Uwekezaji na Maafisa Waandamizi wa Benki Kuu za SADC, utakaofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 12-14 Julai, 2020.
Mkutano ujao unatarajiwa kufanyika Julai 2022, chini ya Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Malawi, ambae atakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa SADC.
No comments:
Post a Comment