Miss Utalii Njombe ang'ara Baiskeli Majimaji Selebuka msimu wa saba
NA MWANDISHI WETU
MSIMU wa saba wa Tamasha la Majimaji Selebuka umemalizika kwa kufana katika Uwanja wa Majimaji mjini hapa, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge.
Tamasha la Majimaji Selebuka lilifanyika kwa siku nane huku likishirikisha Michezo ya Baiskeli, Mdahalo kwa shule za sekondari, burudani za Ngoma za asili, Bongo fleva na vikundi vya kunengua, Maonyesho ya Biashara na Wajasiriamali sambamba na Utalii wa ndani, likiwa chini ya uratibu wa Taasisi ya Songea Mississippi (SOMI), ikishirikiana na Shirika la Maendeleo na Uwezeshaji la Mpingo (MCDI).
Katika Mbio za Baiskeli kwa wanawake Km. 30 ilishuhudiwa Miss Utalii kutoka Njombe, Zawadi Mwambi akiibuka kidedea huku akifuatiwa na Asha Omary kutoka Peramiho nafasi ya pili huku nafasi ya tatu ikienda kwa Paulina Ngonyani pia wa Peramiho.
Kwa upande wa wanaume Km. 100 mshindi akiibuka Ombeni Mbilinyi wa Iringa akifuatiwa na Hagai Sanga wa Mbeya na nafasi ya tatu ikienda kwa Ipyana Mbogela kutoka Iringa.
Kwenye Mdahalo ambako mada ilikuwa 'Misitu Ni Uchumi' washindi waliibuka Songea Girls wakifuatiwa na Songea Boys huku nafasi ya tatu ikienda kwa vijana machachari wa Mashujaa Sekondari.
Washindi walikabidhiwa Zawadi za fedha taslimu, vikombe, medali, vyeti na kwa upande wa Baiskeli walioshika nafasi sita za juu waliongezewa mavazi mà alumu (jezi), za mchezo huo zilizotolewa na kampuni ya Mantra Tanzania.
Pia ulikuwepo Utalii wa Baiskeli ambapo washiriki wakiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Songea Mjini, Dr. Damas Ndumbaro sambamba na Mmiliki wa Taasisi ya Upendo kutoka Arusha, walikuwa ni kivutio katika Zoo ya Ruhila mjini Songea.
Pia zilifanyika hafla za nyama choma pori katika Milima ya Matogoro na Hifadhi ya Ruhila chini ya Mamlaka ya Misitu (TFS), na Mamlaka ya Usimamizi ya Wanyamapori (TAWA).
Kwenye Maonyesho washiriki 17 wakijitokeza zikiwemo Idara za Maliasili na Utalii na Wajasiriamali mbalimbali.
Akizungumza katika hafla ya ufungaji, RC Ibuge, aliwapongeza Waandaaji wa tamasha hilo na washiriki wote huku akihimiza wananchi wa Ruvuma kuwa wakijitokeza kwa wingi katika tamasha hilo linalofanyika kila mwaka.
Aidha alizitaka Taasisi na vikundi washiriki, kuanzisha huduma zao mkoani Ruvuma ili kuchochea Maendeleo ya Mkoa na nchi kwa ujumla.
Miss Utalii Njombe, Zawadi Mwambi.
No comments:
Post a Comment