Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri nchini kutoa kipaumbele cha mikopo kwa wahitimu wa ufundi stadi ili kuwawezesha kujiajiri na kuajiri wengine.
Waziri Mhagama ameyasema hayo Jumamosi, tarehe 31 Julai, 2021, alipotembelea na kukagua shughuli za utekelezaji wa programu ya mafunzo ya Uanagenzi inayofadhiliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu katika Chuo cha VETA Busokelo, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
“Nawaomba sana viongozi wa mikoa na halmashauri mtoe kipaumbele cha mikopo kwa kwa hawa vijana ili wapate mitaji na vifaa vya kufanyia kazi baada ya kuhitimu. Tena ukiwapa hawa watachangia kuongeza mapato kwenye halmashauri yako na unakuwa na uhakika wa mikopo yako kurejeshwa, maana tayari wana ujuzi,” amesema.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwezesha vijana kupata mafunzo ya ufundi stadi na ameahidi kuwa Mamlaka itahakikisha vijana hao wanapata mafunzo bora yatakayowawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa programu hiyo katika Chuo cha VETA Busokelo, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Wilbert Bendera, amesema jumla ya vijana 173 wa Halmashauri ya Busokelo walipata fursa ya mafunzo hayo katika fani za Useremala, Ushonaji, Umeme, Matumizi na Ukarabati wa Kompyuta na Utengenezaji Vifaa vya Kielektroniki, ingawa hadi sasa walioripoti ni 127 tu, sawa na asilimia 74.
Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Mhagama ameagiza uongozi wa Chuo hicho kushirikiana kwa karibu na Mbunge wa Jimbo la Busokelo, Uongozi wa Halmashauri ya Busokelo, pamoja na Diwani wa Kata ya Lufilyo kuhakikisha nafasi za vijana ambao hawakuripoti zinajazwa mara moja ili wana-Busokelo wanufaike na fursa hiyo.
No comments:
Post a Comment