HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 20, 2021

ACT yazoa wanachama Chadema

Wanachama wa Baraza la wanawake Chadema (Bawacha) wakionyesha kadi zao baada ya kujiunga na ACT-Wazalendo, Septemba 19,2021


Na Mwandishi Wetu, Mkuranga


Uongozi wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kata ya Dondo, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, wamejiondoa kwenye chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo.


Mbali na hao, pia wanachama wote wa tawi la Chadema lililopo Kijiji cha Mbafu,Kata ya Dondo  wamejiunga na ACT Wazalendo.


Katika orodha hiyo,  pia yumo aliyekuwa mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia Chadema mwaka 2020, Masudi Daruwesh ambaye mpaka anajiondoa kwenye chama hicho alikuwa Katibu wa Bavicha Pwani -Kusini na mjumbe wa Kamati ya Chadema ni msingi Kanda ya Pwani.


Akitangaza uamuzi huo kwa waandishi wa habari jana Septemba 19,2021, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kata ya Dondo, Abassi Ndambwe alisema wamechukua uamuzi huo baada ya uongozi wa Chadema ngazi za juu kufuata nyayo za CCM kwa kuwatelekeza tangu  Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.


Alisema kwakuwa wao ni wanamageuzi halisi wameamua kuendelea na mapambano ya kudai haki na mapinduzi ya kweli ya fikra kupitia ACT Wazalendo.


Ndambwe alisema tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka jana 2020 wagombea wa vyama vingine  hawajawahi kuwatembelea isipokuwa ACT Wazalendo kupitia kwa aliyekuwa mgombea wake wa Ubunge wa Jimbo la Mkuranga, Mohamed Mtambo ambaye amekuwa nao bega kwa bega  wakati wote. 

Alisema licha ya Mtambo kutokufanikiwa kushinda ubunge, hajakata tamaa bali ameendelea kuwajulia hali na kubadilishana nao mawazo kwa kila hali.


"Sisi lengo letu ni lile lile la kuunganisha umma kujua haki zao kupitia mageuzi ya kifikra na hatimaye kuiondoa CCM madarakani, tunaamini kupitia ACT Wazalendo malengo hayo yatatimia.


"Kwa hakika kabisa tumeamua kuendeleza mapambano ya siasa za ushindani kupitia kwa vyama vya upinzani kwakuwa tunaamini huko ndiko palipo na ukweli daima.


Aidha aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Bawacha Tawi la Mpafu,Zabibu Mlawa alisema wanawake wanaounga mkono vyama vya upinzani wamekuwa wakibaguliwa na Serikali za vijiji hususani katika kupata mikopo kupitia ya kujikwamua kimaendeleo.


Hata hivyo alisema licha ya ubaguzi huo, hawajakata tamaa kwakuwa wanajua wapo kwenye haki.


Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea Ubunge kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Mohamed Mtambo aliwapongeza wanachama hao kwa uamuzi huo wa kuendeleza mapambano ya kisiasa kupitia vyama vya upinzani.


Alisema hatua ya wanachama hao kuhitaji mabadiliko  inampa nguvu na hali ya kuendelea kuwahudumia wananchi wa Mkuranga licha kwamba hakushinda ubunge wa jimbo hilo.


"Wananchi hawa wa Kata ya Dondo walinipigia kura nyingi, nami nimeona ni jambo jema kuja kuwashukuru na kujua changamoto zao ili tutafute namna nzuri ya kuzitatua.


"Kwa mfano, kuna hili suala la watu kubaguliwa kupata mikopo kwa kigezo cha itikadi za kisiasa, hili si sawa, hawa ni wananchi haki zao zinalindwa na Katiba ya Tanzania kuwanyima mkopo na haki Zingine ni uvunjwaji wa haki na tutakwenda kufuatilia hilo suala pale Halmashauri ya Mkuranga."alisema Mtambo.

No comments:

Post a Comment

Pages